Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Ndasi ya Sayansi ya Kompyuta na Elimu ya Masafa wametoa elimu kwa waheshimiwa madiwani na wataalam wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa ajili ya kuwajengea uwezo juu ya matumizi ya takwimu za mfumo rahisi wa kuboresha usimamizi wa ardhi kwa maendeleo ya Jiji la Dodoma.
Akifungua mafunzo hayo Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Prof. Davis Mwamfupe amesema lengo la mafunzo haya ni kuwajengea waheshimiwa madiwani uwezo wa kufanya maamuzi yanayohusu matumizi ya rasilimali ardhi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
"Ili kuweza kutuongezea nguvu za maamuzi tumeona hii warsha ni ya muhimu sana kwani itatufanya tuwe na nafasi ya kutoa maamuzi ambayo yamejikita katika takwimu". Alisema Prof. Mwamfupe.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma Daktari Hektor Mongi amesema mafunzo haya yameratibiwa na Kituo cha Kimataifa cha Wataalam katika Kilimo (CTA) ili kuwafundisha madiwani na wataalam wa Jiji kuhakikisha Jiji la Dodoma linapangwa vizuri na liendeshwe kwa kutumia mifumo ya teknolojia na takwimu.
Neema Mwaluko, Diwani wa Kata ya Kilimani amesema mafunzo haya yatarahisisha upangaji wa mji kupitia 'master plan' inayopitiwa upya, mpango huu utasaidia kupitia na kuboresha makazi maeneo ambayo bado hayajapimwa kama vile Mtaa wa Chinyoya.
Ongezeko kubwa la watu wanaohamia Dodoma wanaathiri sana mipango miji, hivyo juhudi kubwa zinatakiwa kuwekezwa kwenye kujua takwimu za ardhi na kutambua miundombinu ya barabara, shule, vituo vya afya na huduma za maji ili kukidhi mahitaji halisi ya watu kutokana na ongezeko hilo. Amesema Yona Kusaja Diwani wa Kata ya Kikombo.
Hata hivyo, madiwani wameomba warsha za kuwajengea uwezo wa kusimamia uboreshaji wa Jiji la Dodoma ziwepo mara kwa mara ili kupambana na changamoto za ongezeko la kasi ya watu wanaohamia jijini Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.