Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewashukuru viongozi wa dini na Watanzania wote kwa kuitikia wito wa kumuomba Mwenyezi Mungu aepushe janga la ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19).
Mhe. Rais Magufuli alitoa shukrani hizo tarehe 07 Juni, 2020 alipokaribishwa kuwasalimu Waumini wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Bikira Maria Imakulata, Chamwino Mkoani Dodoma baada ya kuhudhuria Misa Takatifu ya Sikukuu ya Utatu iliyoongozwa na Paroko wa Parokia hiyo Padre Paulo Mapalala.
Mhe. Rais Magufuli alisema Mwenyezi Mungu amejibu maombi ya Watanzania ambao wamesali, wamefanya toba na kufunga, na matokeo yake ni kuwa maambukizi ya virusi vya Corona yamepungua, na wananchi wanaendelea na maisha yao huku wakichapa kazi za uzalishaji mali, tofauti na ilivyodhaniwa kuwa ugonjwa huo ungesababisha madhara makubwa.
Alitoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kuwa makini dhidi ya mbinu zozote zinazoweza kufanya kuwaambukiza ugonjwa huo ama magonjwa mengine, huku wakimshukuru na kumtumaini Mwenyezi Mungu aliye mwema wa yote.
"....niwashukuru watanzania wote, wa madhehebu yote ambao katika kipindi cha muda mrefu kidogo tulikaa na kusali na kumuomba Mwenyezi Mungu atuokoe na janga ambalo linalikabiri taifa letu na dunia nzima, ninawashukuru Watanzania kwa sababu, naamini mlikubaliana nami kumtanguliza Mungu katika janga hili, na kwa kweli Mungu amejibu. Palipo na Mungu hakuna kinachoshindikana na ndio maana nasema kwa niaba ya Serikali niwashukuru Watanzania wote, wote wote wote kabisa wa madhehebu yote ambao wengi walifunga, wengi walitubu, wengi walisali na kuswali kwa ajili ya kumtanguliza Mungu mbele, na mimi naamini na ninauhakika Watanzania wanaamini kwamba ugonjwa wa Corona katika nchi yetu umeondolewa kwa nguvu za Mwenyezi Mungu" alisema Rais Dkt. John Magufuli.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.