Na. Getruda Shomi, DODOMA
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru aeleza namna uhakiki wa wamachinga unavyofanywa bila upendeleo kwa kuwasajili wafanya biashara wadogo (Machinga) ili waweze kufanya biashara zao katika soko la wazi la Machinga.
Aliyasema hayo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari katika ukumbi mdogo wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma akiwapa mrejesho kuhusu kukamilika kwa ujenzi wa soko la wazi la Machinga lililopo eneo la Bahi road jijini hapa.
Mafuru alisema kuwa hakuna upendeleo wowote uliofanyika katika kusajili wamachinga na waliosajiliwa ni wamachinga wakweli wasio na maeneo rasmi yakufanyia biashara zao. Usajili huo umewashirikisha viongozi wa Machinga ili kuhakikisha hakuna Machinga anayesajiliwa kinyume na taratibu.
“Tumekaa na uongozi wa wamachinga, na kufanya nao uhakiki na sasa tunaendelea kufanya uhakiki wa mwisho ili waingie wamachinga wa kweli. Tuliwashirikisha kwasababu tukiweka machinga feki wataendelea kubaki kwenye maeneo yasiyo rasmi” alisema Mkurugenzi Mafuru.
Aliongeza kuwa wamachinga wote wamesajiliwa na kupewa namba na vitambulisho vitakavyowatambulisha wao na biashara zao. Hivyo, watakuwa na uwezo wakukopesheka kwasababu watakuwa wanatambulika kwa eneo wanalofanyia kazi na taarifa zao zimehifadhiwa.
Mkurugenzi Mafuru alisema kuwa kwa sasa soko limekamilika kwa asilimia 100 na wamachinga waliosajiliwa waanze kuhamishia biashara zao katika soko hilo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.