Na. Dennis Gondwe, DODOMA
UHIFADHI na utunzaji wa mazingira ni wajibu wa jamii nzima kwa lenygo la kujiondoa katika wimbi la umasikini na kujiletea maendeleo nchini.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri Mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Pinda aliyekuwa mgeni rasmi katika zoezi la kupanda miti katika shule ya Sekondari Nala iliyopo jijini Dodoma leo.
Mhe. Pinda alisema kuwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imesisitiza sana umuhimu wa uhifadhi na utunzaji wa mazingira hasa kupanda miti. “Tanzania ni taifa linaloamini katika kilimo kuwa kitatutoa katika umasikini. Ukijani ndiyo uchumi wenyewe. Uchumi wa kijani, ndio kwetu lazima tukubali kuwa ni jambo kubwa ambalo lazima tulisimamie vizuri. Kazi tuliyonayo sasa kama vijana wa CCM na CCM yenyewe ni kuhakikisha kwamba taifa hili tunalijengea mazingira ambayo yana miti ya kutosha kama mchango wetu katika kuhakikisha dunia inaendelea. Kila mwenyekiti wa shina apande angalau miti mitatu na kuhimiza upandaji miti katika mashina” alisema Mhe. Pinda.
Aidha, aliwataka viongozi wa CCM kupeleka ujumbe wa kupanda miti kwa watu wote. “Miti maji isipandwe karibu karibu, mti mwingine mzuri ni mwarobaini. Wito wangu makampuni binafsi yafikirie kuwezesha upatikanaji wa miti ili iweze kutolewa bila malipo” alisema Mhe. Pinda.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweli alisema “lazima tuwekeze kwenye taaluma ili vijana hawa wafaulu waje kuwa kama Mkurugenzi wa Fedha wa PSSSF mwanamama si ndiyo jamani! lakini pia wapate ajira kwenye viwanda vinavyokuja kujengwa Dodoma” Haitatokea muujiza kama hatuwekezi kwenye elimu. Kwa hiyo niwaombe sana wazazi, chama kwenye ngazi ya Kata, Tawi na Shina pamoja na agenda zingine, agenda ya mazingira na elimu ziwe agenda za kudumu kuhamasisha watu wetu wasome na kushiriki katika uchumi wa makao makuu ya nchi” alisema Shekimweli.
Zoezi la upandaji miti katika shule ya sekondari Nala iliyopo katika Kata ya Nala liliongozwa na Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya, Katibu wa CCM Wilaya, Mbumbe, Diwani wa Kata, Madiwani wa Viti hMaalum, maafisa waandamizi kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma na Jumuiya ya Shule ya Sekondari ya Nala ambapo jumla ya miti 700 ilipandwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.