Na. Theresia Nkwanga, HOMBOLO MAKULU
KAMATI ya Siasa ya Mkoa wa Dodoma imeridhishwa na viwango vya ujenzi wa nyumba ya walimu ‘two in one’ katika Shule ya Sekondari Mtemi Chiloloma na kusema kuwa utakuwa imejengwa kwa viwango bora.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma, Pili Mbaga alipoongoza Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Dodoma kutembelea na kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mbaga alisema kuwa Kamati ya Siasa Mkoa wa Dodoma imeridhishwa na ujenzi wa nyumba ya walimu shuleni hapo. “Mradi wa ujenzi wa nyumba ya walimu ni mzuri na umejengwa na kusimamiwa vizuri. Huko zamani wahandisi walikuwa nyuma katika kusimamia miradi ya ujenzi, lakini siku hizi wapo mstari wa mbele na wanafika katika kusimamia miradi ya ujenzi. Jukumu letu ni kuwaambia wananchi kazi nzuri inayofanywa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hapa tumeambiwa zilitolewa shilingi 95,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya walimu ‘two in one’ na sasa zimeletwa shilingi 216,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya kidato cha tano na sita” alisema Mbaga.
Akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa nyumba ya walimu kwa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Shule ya Sekondari Mtemi Chiloloma, Mwl. Livinus Tangayika alisema kuwa serikali kupitia mradi wa kuboresha shule za sekondari (SEQUIP) ilitoa jumla ya shilingi 95,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya walimu ambapo lilikuwa ni hitaji kubwa kwa sababu eneo la shule liko mbali na eneo la makazi ya watu. Fedha za ujenzi ziliingizwa katika akaunti ya shule tarehe 20/6/2023 na kuvuka mwaka na kuanza kutumika katika mwaka wa fedha 2023/2024.
Akiongelea utekelezaji wa mradi huo alisema kuwa ulianza tarehe 9 Septemba, 2023 baada ya taratibu za manunuzi kukamilika na ujenzi unatekelezwa kupitia ‘force account’. “Mradi huu unahusisha ujenzi wa nyumba moja ya walimu (two in one) yenye vyumba vitatu, sebule, jiko na stoo kwa kila nyumba. Utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 99 ikiwa bado milango michache ambayo ipo kwa fundi katika hatua ya umaliziaji pamoja na ufungaji wa vyoo viwili vya kukaa. Mradi unategemea kukamilika kabla au ifikapo tarehe 25 Novemba, 2023 tayari kwa matumizi” alisema Mwl. Tanganyika.
Kuhusu faida za mradi ukikamilika, alizitaja kuwa ni walimu kukaa kwenye mazingira ya shule na hivyo kuongeza ufanisi katika utendaji kazi. Nyingine ni kuwezesha mazingira mazuri ya kuishi kwa walimu, aliongeza.
Ikumbukwe kuwa ujenzi wa Shule ya Shule ya Sekondari Mtemi Chiloloma umetumia kiasi cha shilingi 94,823,000 hadi wakati Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Dodoma inaitembelea.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.