MRADI wa ujenzi wa kituo cha kisasa cha mabasi unaojengwa katika Halmashauri ya jiji la Dodoma umefikia asilimia 59 na kuwafanya wakazi na wageni kufurahia hatua hiyo.
Hayo yamesemwa na Mhandisi mshauri wa mradi huo, Mhandisi Emmanuel Mahimbo alipokuwa akitoa taarifa fupi ya hali ya ujenzi wa mradi huo kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mwita Waitara ambaye amefanya ziara ya kutembelea mradi huo leo.
Mhandisi Mahimbo alisema “hadi sasa mradi wa ujenzi wa kituo cha kisasa cha mabasi umefikia asilimia 59”. Kazi kubwa inayoendelea ni ujenzi wa sehemu ya juu ya jengo hilo na kupanda bustani za maua, aliongeza. Kazi nyingine alizitaja kuwa ni ujenzi wa barabara za kuingia na kutoka katika kituo hicho pamoja na kuweka ‘paving blocks’. Mhandisi huyo mshauri, alimtaarifu Naibu Waziri kuwa ujenzi huo hauna changamoto yoyote katika utekelezaji wake. Akiongelea matarajio ya kumalizika mradi huo, alisema kuwa ifikapo mwezi Septemba, 2019 utakuwa umekamilika.
Nae Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alisema kuwa kituo hicho cha kisasa cha mabasi kinajengwa katika eneo lenye ekari 60 kikiwa na uwezo wa kuhudumia watu 4,000 kwa wakati mmoja. “Mradi wa kituo cha kisasa cha mabasi na soko la kisasa kwa pamoja imegharimu zaidi ya shilingi bilioni 35 zikiwa ni fedha kutoka serikali kuu ambazo ni mkopo wa benki ya dunia” alisema Kunambi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Waitara alipongeza maendeleo ya miradi hiyo mikubwa ya kimkakati na kusema kwamba italifanya jiji la Dodoma kuonekana jipya na tofauti.
Ikumbukwe kuwa mkataba wa ujenzi wa kituo cha kisasa cha mabasi cha halmashauri ya jiji la Dodoma kilichopo katika kata ya Nzuguni ni miezi 15 kuanzia mwezi Julai, 2018.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.