Kamati ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeridhishwa na hali ya ujenzi inayoendelea katika shule ya msingi Mnyakongo iliyopo kata ya Nkuhungu jijini hapa.
Kauli hiyo ilitolewa na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe baada ya kuongoza kamati ya fedha na utawala kutembelea na kukagua vyumba vitatu vya madarasa katika shule ya msingi Mnyakongo jana.
Akiongea na wajumbe wa kamati ya fedha na utawala na wajumbe wa kamati ya ujenzi ya shule hiyo, Mstahiki Meya alisema kuwa kazi ya ujenzi iliyofanywa katika shule hiyo ni nzuri. “Nawapongeza wanaosimamia ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa katika shule hii. Kazi iliyofanywa hapa ni nzuri. Katika madarasa haya wekeni picha mbalimbali na ramani ili madarasa yawe yanaongea” alisema Prof. Mwamfupe. Aliitaka menejimenti ya Halmashauri kuangalia utaratibu wa kuwapongeza watumishi waliosimamia mradi wa ujenzi wa shule na utunzaji wa fedha katika mradi huo kutokana na kazi kubwa na nzuri waliyofanya. Alipongeza uzalendo unaofanywa na watumishi hao kwa lengo la kuhakikisha miradi hiyo itatekelezwa vizuri kwa mujibu wa mipango iliyopo.
Aidha, aliishauri shule hiyo kupanda miti kuzunguka eneo lote la shule. “Shule hii haina miti, miti inatakiwa kupandwa katika maeneo ya shule ili kutunza mazingira na kupendezesha shule” alisema Prof. Mwamfupe.
Akielezea hali ya utekelezaji wa mradi huo, Mchumi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Happiness Matonya alisema kuwa Halmashauri hiyo ilipeleka tofali 5,100 zilizotolewa na Waziri mkuu shuleni hapo kwa ajili ya ujenzi. Kiasi cha shilingi 15,000,000 zilitolewa na Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kutoka mapato ya ndani kwa aili ya ujenzi wa shule hiyo. Mchumi, aliendelea kufafanua kuwa mpango wa Halmashauri ni kukamilisha madarasa yanayoendelea kujengwa na kuanza ujenzi wa madarasa mengine manne. “Mstahiki Meya, katika bajeti ya mwaka 2019/2020 Halmashauri ya Jiji imetenga shilingi milioni 200 katika bajeti yake kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo, ofisi, umeme na maji” alisema Matonya.
Kwa upande wake, mjumbe wa kamati hiyo, Mhe. Paskazia Mayala alisema kuwa katika mipango ya ujenzi wa shule hiyo suala la viwanja kwa ajili ya michezo ya wanafunzi lizingatiwe. “Mstahiki Meya, viwanja vya michezo vipewe kipaumbele kwa sababu michezo ni muhimu kwa afya za wanafunzi na pia ni sehemu ya masomo yao” alisema Mayala.
Wajumbe wa Kamati ya Fedha na Uongozi wakiwa na wataalam wa Jiji la Dodoma, kamati hiyo ilipofanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ya Jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.