Na. Dennis Gondwe, DODOMA
UJENZI wa darasa na chumba cha ofisi umefikia hatua ya kuweka kifusi kwenye msingi ili kufunga jamvi katika shule ya sekondari Dodoma.
Kauli hiyo ilitolewa na Mratibu wa mradi wa ujenzi wa chumba cha darasa na ofisi ndogo, Mwl. Abdallah Ngesa katika shule ya sekondari Dodoma iliyopo Kata ya Makole Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mwl. Ngesa alisema “tarehe 1/10/2022 tulipokea shilingi 20,000,000 kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa ajili ya ujenzi wa chumba kimoja cha darasa, ofisi na samani zake. Mkuu wa shule alifanya kikao cha menejimenti ya shule kutoa taarifa ya mapokezi ya fedha. Baada ya hapo bodi ya shule ilitaarifiwa kiasi hicho cha fedha kilichopokelewa kwa ajili ya ujenzi. Tulimuandikia barua Diwani wa Kata na Afisa Mtendaji wa kata na Mwenyekiti wa mtaa kuwajulisha pia”.
Alisema kuwa shule hiyo ilipokea barua kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma ikionesha Mkurugenzi wa Jiji kukasimisha madaraka kwa Mkuu wa shule ya sekondari Dodoma kusimamia ujenzi na taratibu za kimuongozo za kufuata katika ujenzi huo. Mkuu wa shule aliunda kamati tatu kwa mujibu wa muongozo wa kusimamia ujenzi. “Kamati ya kwanza ni usimamizi na utekelezaji wa mradi, kamati ya manunuzi na kamati ya ukaguzi wa vifaa na mapokezi. Kamati zote zinawajumbe watano kila mmoja. Hatua iliyofuata tulitoa tangazo la kazi ili kualika mafundi kuomba kazi ya ujenzi. Mafundi watatu waliomba kazi hiyo. Tarehe 13/10/2022 kikao cha tathmini kilifanyika na kumuidhinisha fundi mmoja aliyekidhi vigezo. Tarehe 14/10/2022 kikao cha menejimenti ya shule kilifanyika kumuidhinisha fundi na vifaa vya ujenzi” alisema Mwl. Ngesa.
Ujenzi wa darasa na ofisi ndogo umefikia hatua ya kuweka kifusi katika msingi ili kuruhusu ufungaji wa jamvi wakati ujenzi ukitarajiwa kukamilika ndani ya siku 20 zijazo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.