WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua wa awamu ya pili ya ujenzi wa Ofisi za Wizara katika Mji wa Serikali uliopo eneo la Mtumba jijini Dodoma na ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango ihakikishe kuwa fedha kwa ajili ya mradi huo zinapatikana kwa wakati na kikamilifu.
Mheshimiwa Majaliwa ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Desemba 2, 2021) baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora ikiwa ishara ya uzinduzi wa awamu ya pili ya ujenzi wa Ofisi za Wizara katika Mji wa Serikali.
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha shilingi bilioni 300 ili zitumike katika ujenzi wa Ofisi za Wizara na miundombinu mbalimbali itakayojengwa katika Mji wa Serikali na Jiji la Dodoma.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kwamba awamu ya kwanza ya ujenzi wa ofisi 23 za Serikali ulianza tarehe 28 Novemba, 2018 na kukamilika tarehe 22 Machi, 2019 ambapo Shilingi bilioni 39.387 zilitumika kwa ajili ya awamu ya kwanza ya ujenzi huo.
“Watumishi zaidi ya 18,300 wa Serikali Kuu, Bunge, Vyombo vya Ulinzi na Usalama na baadhi ya Taasisi wamehamia Dodoma ambapo kiasi cha shilingi bilioni 162.123 kimetumika kwa ajili ya gharama za posho za uhamisho, ununuzi na usafirishaji wa vifaa, ukarabati na ujenzi wa miundombinu wezeshi ya ofisi.”
Uzinduzi wa huo wa awamu ya pili ya ujenzi wa Ofisi za Wizara na miundombinu mbalimbali zinazojengwa katika Mji wa Serikali ni miongoni mwa matukio ya maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania ambayo kitaifa yatafanyika mkoani Dar es Salaam Desemba 9, 2021.
Amesema uzinduzi huo ambao utahusisha majengo 24 ya ghorofa unalengo la kuwa na Mji wa Serikali wa kisasa utakaozingatia dhana ya Mji wa Kijani na mji rafiki ili kudhibiti gharama za kiuendeshaji za Serikali za majengo hayo ikiwemo kuzingatia matumizi ya nishati mbadala.
“Awamu ya pili ya ujenzi wa ofisi za Wizara itakwenda sambamba na ujenzi wa miundombinu muhimu ya kudumu ya maji, umeme, mawasiliano, usalama, gesi, TEHAMA, zimamoto na uokoaji, programu za upandaji miti pamoja na ujenzi wa huduma mbalimbali za kijamii.”
“Katika utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais Samia la kuzitaka Wizara kuanza ujenzi mara moja, ninafurahi na kufarijika kuona kwamba tayari Wizara zote zimeshakamilisha taratibu za manunuzi za kuwapata wakandarasi na washauri elekezi wa ujenzi.”
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.