MKUU wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Dkt. Binilith Mahenge amesema mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma utakapokamilika utarahisisha usafirishaji wa vifaa vya ujenzi na kuwezesha gharama za ujenzi kupungua Mkoani humo.
Ametoa kauli hiyo alipokuwa akiukaribisha ujumbe wa wageni nane kutoka Jiji la Linz la nchini Austria mjini hapa leo Februari 12, 2018, ukiongozwa na Meya wa Jiji hilo la Linz.
“Reli hii ya kisasa itakapokamilika itarahisisha usafirishaji wa vifaa vya ujenzi na kuwezesha gharama za ujenzi kupungua” alisema Mhe. Dkt.Mahenge.
Dkt. Mahenge alisema kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. John Magufuli imefanikisha dhamira ya kuhamishia Serikali mjini Dodoma na kuufanya Mji huo kuwa Makao Makuu ya Nchi kwa vitendo.
“Dhamira hii ilianzishwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere Mwaka 1973 na imetekelezwa na Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt. Magufuli” alisema Mhe. Dkt. Mahenge.
Alisema, katika utekelezaji wa dhamira hiyo, Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi, ikiwemo reli ya kisasa ya kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ambayo baadaye ujenzi wake utaendelea hadi mkoani Mwanza, na kwamba kukamilika kwa mradi huo kutarahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo.
Mheshimiwa Dkt. Mahenge aliueleza ujumbe huo kuwa, Mkoa wa Dodoma una miradi mingi ya ujenzi kutokana na Serikali kuhamia, ikiwemo miradi ya ujenzi wa Ofisi mbalimbali na nyumba za makazi pamoja na miundombinu.
Awali, Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Mhe. Prof. Davis Mwamfupe alisema kuwa ziara hiyo ya Mstahiki Meya wa Jiji la Linz inalenga kuendeleza ushirikiano baina ya Jiji lake na jiji la Linz la nchini Austria.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.