HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeongoza ukusanyaji wa mapato ya ndani katika kipindi cha miezi tisa kwa kukusanya shilingi bilioni 36.04.
Akitoa taarifa ya mapato na matumizi ya Halmashauri, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Selemani Jafo wiki iliyopita alisema kuwa katika kipindi cha miezi tisa (Julai, 2019 – Machi, 2020), Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilikusanya shilingi bilioni 36.04.
Waziri Jafo alisema “ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri kwa kuzingatia wingi wa makusanyo ni Jiji la Dodoma ambalo limeongoza kundi la Majiji kwa kukusanya Shilingi bilioni 36.04 na Jiji la Dar es Salaam limekuwa la mwisho ambapo limekusanya Shilingi bilioni 8.83”.
Kwa upande wa Manispaa, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imeongoza kwa kukusanya Shilingi bilioni 43.14 na Manispaa ya Kigoma Ujiji imekuwa ya mwisho katika kundi hilo ambapo ilikusanya Shilingi Bilioni 1.20 aliongeza Mhe. Jafo.
Aidha, Halmashauri ya Mji wa Geita iliongoza kwa wingi wa mapato kwa kukusanya Shilingi Bilioni 7.02 na Halmashauri ya Mji wa Mbulu ilikuwa ya mwisho katika kundi hilo kwa kukusanya Shilingi Milioni 671.78. “Na kwenye Halmashauri za Wilaya, Halmashauri ya Chalinze imeongoza kwa kukusanya mapato mengi ya Shilingi Bilioni 5.78 na Halmashauri ya Wilaya ya Gairo ilikuwa ya mwisho katika kundi hili ambapo ilikusanya Shilingi Milioni 343.70” alisema Waziri Jafo.
Ikumbukwe kuwa kwa mwaka wa fedha 2019/20 Halmashauri zilipanga kukusanya shilingi bilioni 765.48 kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani na katika kipindi cha Julai, 2019 hadi Machi, 2020 Halmashauri zilikusanya jumla ya Shilingi bilioni 527.31 ambayo ni asilimia 69 ya makisio ya mwaka.
Kwa habari zaidi bofya hapa: Ukusanyaji Mapato ya Ndani
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.