Akiyekuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa serikali ya awamu ya tano kipindi cha kwanza, Ummy Mwalimu ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuwa na uwanja wa kisasa kwa ajili ya mchezo wa mpira wa kikapu.
Mwalimu ambaye pia ni Mbunge wa Tanga Mjini aliyasema hayo leo alipotembelea Bustani ya Mapumziko ya Chinangali jijini hapa yanaponedelea mashindano ya kitaifa ya mpira wa kikapu “CRDB Bank Taifa Cup”.
Mbunge Ummy aliyewasili katika bustani hiyo majira ya saa 6:37 mchana kwa ajili ya kuishangilia timu ya Mkoa wa Tanga inayoshiriki mashindano hayo, alisema kuwa viwanja vya mpira wa kikapu ni moja ya viwanja bora nchini. Napenda kulipongeza Jiji la Dodoma kwa kuwa na viwanja vizuri kiasi hiki.
Aidha, Mbunge huyo aliishauri Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuangalia jinsi ya kuongeza vivutio ili kuwawezesha wananchi wengi kufika eneo hilo kwa ajili ya mapumziko ikiwepo nyama choma.
Pamoja na Mbunge huyo wa Tanga mjini, wabunge wengine kutoka mkoa wa Tanga waliotembelea mashindano hayo kutoka Mkoa wa Tanga ni Hamis Mwinjuma (Muheza), Jumaa Aweso (Pangani).
Ikumbukwe kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ndiyo Halmashauri pekee nchini yenye bustani ya kisasa ya aina yake na inatarajia kufanya mnada wa hadhara wa kumpata muwekezaji wa kuendesha eneo la Bustani ya Mapumziko ya Chinangali tarehe 21 Novemba, 2020 saa 3:00. Bustani hiyo ina viwanja vya kisasa kwa ajili ya mchezo wa mpira wa kikapu, tenisi, wavu, mabwaya ya kuongelea yenye viwango vya Olympic, jukwaa la sanaa na GYM.
Mhe. Ummy Mwalimu (Tanga), Mhe. Hamis Mwinjuma (Muheza) na Mhe. Jumaa Aweso (Pangani), Phares Magesa (kiongozi wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania) wakiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa Timu ya mpira wa Kikapu ya Mkoa wa Tanga kwenye viwanja vya Bustani ya Mapumziko ya Chinangali jijini Dodoma yanapofanyika machindano ya taifa ya mpira wa kikapu. (Picha kwa hisani ya Clouds Digital)
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.