BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) leo Ijumaa, Juni 10, 2022 imezindua rasmi mfumo wa kidigitali unaomwezesha mwajiri kuwasilisha makato na orodha ya wanufaika-wafanyakazi wake kwa njia ya mtandao kutoka popote alipo.
Akizindua mfumo huo jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru amesema mfumo huo ulianza kwa majaribio mwaka 2019/2020 na sasa umekamilika na hivyo kuwawezesha waajiri na wanufaika kurejesha mkopo kwa urahisi.
“Zamani ilikuwa mwajiri inabidi atoke ofisini kwake aje HESLB kufanya malipo lakini kwa sasa anaweza kuwasilisha orodha ya wanufaika-wafanyakazi wake na makato kutoka popote alipo kwa kutumia mfumo wetu huu ambao anajiunga kupitia tovuti yetu (www.heslb.go.tz),” amesema Mkurugenzi Mtendaji Abdul-Razaq Badru.
Kwa mujibu wa Badru, amesema mfumo huo pia unamwezesha mnufaika mmoja mmoja kupata taarifa za deni lake na utaratibu wa kurejesha kupitia tovuti ya HESLB.
“Kuanzia mwaka jana, imekuwa ni rahisi sana, unaingia kwenye tovuti yetu, unabofya ‘rejesha mkopo’ au ‘repay loan’ na kufuata maelekezo ya kujisajili na utaendelea kupata taarifa ya deni lako palepale au hata kudai refund (makato yaliyozidi),” amesema Badru.
Akizungumzia uzoefu wake katika kutumia mfumo huo, mwakilishi wa Shule ya Msingi Young Jai iliyopo jijini Dodoma, Bi. Young Mi Cha ameshauri HESLB iboreshe mfumo kuwawezesha waajiri kuwatambua waajiriwa wapya kama walinufaika na mikopo ya elimu ya juu.
“Kuna wakati waajiriwa wapya wanadanganya, hivyo pamoja na uzuri wa mfumo huu, ninashauri uboreshwe ili mwajiri aweze kutambua mwajiriwa mpya kama ni mnufaika wa HESLB au hapana bila kumuuliza au kuleta jina kwenu kwa uhakiki kwanza,” amesema Bi Young.
HESLB ilianzishwa mwaka 2005 ikiwa na majukumu makuu mawili, kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji wanaojiunga na taasisi za elimu ya juu na kukusanya mikopo iliyoiva kutoka kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu tangu mwaka 1994/1995.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.