Na. Dennis Gondwe, DODOMA
DIVISHENI ya Elimu Sekondari Halmashauri ya Jiji la Dodoma imesema kuwa ushirikiano baina ya Baraza la Madiwani, Menejimenti ya halmashauri na walimu unaifanya divisheni hiyo kutembea kifua mbele katika kuboresha sekta ya elimu na kutoa matokeo mazuri kwa wanafunzi wanaofanya mtihani wa taifa wa kidato cha Nne mwaka 2022.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Divisheni ya Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Upendo Rweyemamu alipokuwa akiongelea umuhimu wa ushirikiano katika kutoa matokeo bora kwa wanafunzi wa sekondari jijini hapa.
Mwalimu Rweyemamu alisema “niwashukuru sana walimu wangu kwa jinsi walivyopambana na kuwapigania wanafunzi wetu wanaofanya mtihani wa taifa wa kidato cha Nne. Niwashukuru sana wakuu wa shule wamekuwa na ushirikiano na divisheni yangu. Hakika mikakati tunayoandaa na kuiteremsha kwao wanatekeleza kwa weledi mkubwa. Mimi kama kiongozi wao niwashukuru sana kwa kazi nzuri na hakika vijana tumewaandaa vizuri” alisema Mwalimu Rweyemamu.
Aidha, alishukuru ushirikiano anaoupata kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma. “Kama mkuu wa divisheni unaweza kuwa na mawazo mazuri ya jinsi ya kuboresha taaluma, lakini usipopata uungwaji mkono wa mkurugenzi huwezi toboa. Mkurugenzi amekuwa msaada mkubwa sana kwetu na hata gharama za wanafunzi na posho za walimu waliokuwa wakiwasaidia wanafunzi hawa amewezesha na kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri. Natamani matokeo ya watoto hawa yawe mazuri ili aweze kupata faraja. Kipekee niwashukuru wajumbe wa Baraza la Madiwani la Jiji la Dodoma wakiongozwa na Mstahiki Meya. Wamekuwa kweli ni msaada mkubwa sana kwenye Divisheni ya Elimu Sekondari. Matunda haya ninayopata siyo kwamba napigana mwenyewe nina nguvu kubwa ya viongozi wangu pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Uchumi na Afya ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma” alisema Mwalimu Rweyemamu.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma ina vituo 54 vitakavyofanya mtihani wa kidato cha Nne, ikiwa na jumla ya watahiniwa 6,647 ambao watafanya mtihani wa taifa wa kidato cha Nne, wavulana wakiwa 3019 na wasichana 3,628.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.