Na. Dennis Gondwe, DODOMA
CHAMA cha Mapinduzi Wilaya ya Dodoma kimepongeza ushirikiano mzuri kati yake na serikali katika utekelezaji wa Ilani na utatuzi wa kero za wananchi.
Pongezi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Dodoma, Meja (Mst.) Johnick Risasi Salingo alipokuwa akitoa salamu katika Baraza maalum la Madiwani lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Mipango jijini Dodoma.
Meja (Mst.) Risasi alisema kuwa Chama cha Mapinduzi na Serikali wanafanya kazi kwa kushirikiana. “Chama na Serikali tumekuwa tukishirikiana kwa karibu sana. Tunashirikiana sana katika kutatua kero za wananchi na utekelezaji wa Ilani. Wito wangu kwa Wakuu wa Idara, chapeni kazi kwa weledi” alisema Meja (Mst.) Risasi.
Akiongelea uteuzi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji, alisema kuwa Mungu ambariki. “Napenda kutoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumteua Joseph Mafuru kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji. Lengo la Mheshimiwa Rais kumteua na kumuacha Dodoma ni ili tushirikiane na katika utekelezaji wa Ilani ya CCM. Mungu akubariki sana, chapa kazi usiwe na hofu, chama kipo pamoja nawe” alisema Meja (Mst.) Risasi.
Akiongelea tahadhari ya ugonjwa wa UVIKO-19, Mwenyekiti huyo alisema kuwa amekwisha chanja. “Mimi nimechanja na nipo katika hali nzuri. Sisi kama viongozi tuwafafanulie wananchi wapate habari njema na kuchanja ni hiari. Ila kufa kwako ni jambo la kwako kwa sababu mambo mengine utayaacha. Viongozi tuwe mstari wa mbele kuonesha mambo mema” alisema Mwenyekiti huyo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.