Na. Dennis Gondwe, DODOMA
KAMATI ya Siasa Wilaya ya Dodoma imeridhishwa na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) unaofanywa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mjini Dodoma (DUWASA) ya kuwasogezea wananchi huduma ya maji.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Dodoma, Meja Mst. Johnick Risasi wakati alipoongoza hiyo kutembelea kituo cha kuzalisha Maji Mzakwe jijini Dodoma.
Meja Mst. Risasi kuwa baada ya kamati ya siasa kutembelea na kukagua kazi inayofanywa na DUWASA imeridhika. “Kamati ya Siasa ya Wilaya imepita kukagua kazi inayofanywa na DUWASA na imejiridhisha na utekelezaji wa miradi ya Maji inayotekelezwa wilayani Dodoma. Nichukue nafasi hii kuwapongeza sana DUWASA kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi” alisema Meja Mst. Risasi kwa uhakika.
Akiongelea uhusiano baina ya upatikanaji wa huduma ya Maji na maendeleo, Mwenyekiti huyo alisema kuwa Maji yanachochea maendeleo. “Ndugu zangu Maji ni uhai, mnatuona tunatakata hapa kwasababu ya Maji. Tuwashukuru sana DUWASA kwa huduma hii nzuri. Bila Maji hatuwezi pata maendeleo. Mtakumbuka kuwa watu walikuwa wanatumia muda mrefu kutafuta huduma ya Maji. Sasa huduma hii inapofikishwa kwa wananchi, wanatumia muda zaidi katika shughuli za maendeleo” alisema Meja Mst. Risasi.
Akitoa maelezo ya hali ya huduma ya maji mjini Dodoma, mwalikishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Sebastian Warioba alisema kuwa hali ya usambazaji ni nzuri. “DUWASA imefanikiwa kuunganisha huduma ya majisafi kwa wateja 56,266 kupitia maunganisho haya, DUWASA imeweza kuhudumia asilimia 62.7 ya wakazi” alisema Warioba.
Warioba alisema kuwa DUWASA imefanikiwa kuondoa mgao mkali wa maji uliokuwepo kabla ya kuanzishwa kwa DUWASA mwaka 1998. “DUWASA imefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya kuboresha huduma ya maji ikiwepo mradi ulioongeza uwezo wa uzalishaji maji Mzakwe kutoka lita milioni 30 kwa siku hadi lita Milioni 61 kwa siku uliokamilika mwaka 2015” alisema Warioba.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Rukia Bakari aliwapongeza DUWASA kwa kazi nzuri ya kusogeza huduma ya maji kwa wananchi. “DUWASA hongereni kwa kazi nzuri. Kweli kazi imefanyika na inaonekana. Huu ni utelekezaji wa Ilani ya CCM ulio wazi. Halmashauri ya Jiji itaendelea kutoa ushirikiano kwa DUWASA ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi zaidi” alisema Bakari.
DUWASA ina mtandao wa majisafi wenye urefu wa Kilometa 687.07.
Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Dodoma, Meja Mst. Johnick Risasi (kushoto) akisisitiza jambo kwa mwalikishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Sebastian Warioba (kulia) wakati Kamati Siasa Wilaya ilipotembelea miradi inayotekelezwa katika Wilaya ya Dodoma, katikati ni mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Rukia Bakari.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.