Na. Hellen M. Minja,
Habari – DODOMA RS
Katika utekelezaji wa kampeni ya ‘Kijanisha Dodoma’, Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma pamoja na Watumishi wa taasisi mbalimbali za Serikali Mkoani hapa,wakiongozwa na Katibu Tawala Mkoa Bw.Kaspar Mmuya, wamepanda miti takribani 988 katika maeneo tofauti Jijini Dodoma.
“Tumeweza kupanda Miti kando kando ya barabara na maeneo ya wazi, lengo likiwa ni kufanya mji wetu wa Dodoma uonekane msafi, uwe na rangi ya kijani,lakini pia barabara hizo zituzwe ili kuzuia mmomonyoko na kupata kivuli” Bw. Mmuya
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir Shekimweri ambaye ameshiriki upandaji miti amesema lengo ni kutunza barabara.
“Tumeona tujielekeze kwenye kuhifadhi barabara zetu na kuzifanya ziwe nadhifu na mandhari nzuri, kwani barabara hizi bado hazijakabidhiwa na zipo kwenye hatua za umaliziaji hivyo tutawasiliana na Wakandarasi ili wafanye kurudisha kwa jamii kwa kuunda vikundi vya uangalizi wa miti hii” Mhe. Shekimweri
Akiongea kwa niaba ya Wakuu wa Taasisi zilizopo katika Mkoa wa Dodoma zilizoshiriki katika zoezi hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa TARURA Mkoa wa Dodoma Mhandisi Edward Dimelo amesema;
“Miti hii ni muhimu kupandwa kwenye barabara kwani inasaidia sana kutunza barabara zetu. Wananchi wanaweza kuwa mashahidi kipindi hiki cha mvua, sehemu nyingi zimekua na mmomonyoko wa udongo kwa sababu hakuna miti ila kwa kupanda miti hii, tunakwenda kuzuia mmomonyoko wa udongo na barabara zetu zitakua katika hali nzuri”
Maeneo yaliyopandwa miti katika utekelezaji wa kampeni hiyo ni pembezoni mwa barabara ya Mlimwa C kuzunguka ukuta wa makazi ya Waziri Mkuu yenye urefu wa Km 2.6 ambao imepandwa miti 588 pamoja na barabara ya Bima yenye urefu wa Km 2 iliyopandwa miti 400.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.