Mfumo wa Ritani mtandaoni utawarahisishia wafanyabiashara nchini - TRA
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imezindua mfumo wa uwasilishaji wa taarifa kwa mlipa kodi na kuwataka wafanyabiashara wote wakubwa nchini kutumia ili kuondokana na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikijitokeza hapo awali.
Akizungumza jijini Dar es Salaam tarehe 19/08/2020, Kamishna wa Walipakodi Wakubwa TRA, Alfred Mregi, alisema kimsingi ujio wa mfumo huo uliozinduliwa rasmi Agosti 6 Mwaka huu, utawasaidia wafanyabiashara pamoja na TRA kuepuka upotevu wa muda pale mwananchi anapotakiwa kupeleka taarifa fulani zinazohusu kodi.
Mregi alisema awali kabla ya kuzinduliwa kwa mfumo huo wateja wao hao ambao ni walipa kodi wakubwa walikuwa wakilazimika kuwasilisha taarifa hizo kwa njia ya kawaida kwa kupeleka taarifa zao moja kwa moja katika ofisi za TRA tofauti na sasa ambapo mteja ataweza kutuma taarifa akiwa mahali popote.
“Kwa sasa wataweza kuwasilisha taarifa zao kutoka mahali popote, hii mbali na kuokoa muda waliokuwa wakiutumia kwenda katika ofisi zetu, pia mfumo huu utawasaidia wafanyakazi wetu kuondokana na hali ya kukosea kosea katika uingizaji wa taarifa hizo katika mfumo wetu hivyo kuathiri makadirio,” alisema Mrige.
Aidha alisema kupitia mfumo huo mpya, wafanyabiashara wataweza kupata majibu ya moja kwa moja ya mapokeo ya kodi yake ndani ya wakati, tofauti na hapo awali ambapo alilazimika kusubiri taarifa pale ambapo itakuwa imeshapigwa muhuri kutoka TRA.
“Kodi inalipwa kutokana na makadirio tunayoyafanya kwa biashara husika, hivyo unapopata taarifa sahihi ndipo hapo utakapoweza kukadiria ipasavyo kuwa ni kiasi gani unapasa kutoza, kimsingi mfumo huu umekuja kama mkombozi katika shughuli nzima ya ukusanyaji wa mapato kwa wafanyabiashara huku tukiamini kuwa hata wao wataufurahia.
Katika hatua nyingine Kamishna huyo wa walipakodi wakubwa aliwakumbusha waajiri wote nchini kuhakikisha wanawakumbusha wafanyakazi wao kuwapatia namba za mlipakodi (TIN) kwa ajili ya utekelezaji wa masuala mbalimbali yanayohitajika na TRA hususani katika kupata taarifa sahihi za watumishi hao ili iweze kuwa na usahihi katika viwango vya kodi inayopasa kuitoza.
Alisema mfumo huo wa uhitaji wa TIN umelenga kuhakikisha waajiri wanatoa taarifa sahihi tofauti na hapo awali ambapo wengi walikuwa wakidanganya na hivyo kusababisha TRA kupata hasara kutokana na kutoza kodi kwa idadi ndogo ya wafanyakazi tofauti na uhalisia kamili.
Chanzo: HabariLeo
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.