JUMLA ya mitaa 222 iliyopo ndani ya kata 41 za halmashauri ya Jiji la Dodoma, zinatarajiwa kuwekewa anuani za makazi ili kurahisisha utoaji wa huduma mbalimbali za kimawasiliano, kiusalama, kiuchumi ikiwemo kukusanya kodi mbalimbali kwa urahisi na kurahisisha kazi za uokoaji na kuzuia maafa wakati wa majanga kama ajali ya moto.
Mratibu wa mfumo wa uwekaji anuani za makazi Jiji la Dodoma Joseph Nkuba alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Jijini humo.
Nkuba alisema kuwa mitaa hiyo itakayowekewa anuani itaongeza ufanisi kwenye mitaa mbalimbali katika kufikisha bidhaa na kuzuia upotevu, na kwa wananchi kurahisisha kutambua makazi yao.
Mratibu huyo alisema zoezi hilo limeshaanza kwa hatua za awali huku akitaja faida zingine za mfumo huo kuwa ni kurahisisha huduma za ulinzi na usalama, kuongeza ufanisi katika usimamizi wa makazi ya watu na kutambua mali na upatikanaji wa takwimu mbalimbali.
Zingine ni kuongeza tija na ufanisi katika huduma za uokoaji na kuzuia maafa, kuwezesha ukusanyaji wa kodi mbalimbali kwa urahisi na kwa wakati ikiwa na pamoja na kupambana na uhalifu katika kupata taarifa za uhamiaji na shughuli za utalii.
“Uwekaji wa anuani za makazi ulianza katika hatua za awali Disemba 13, 2021 kwa kutambua mipaka ya mitaa 153 na hadi sasa iliyobaki ni mitaa 69 na itakamilishwa ifikapo Mei 22 mwaka huu.
“Pia katika kuhakikisha zoezi hilo linakamilika kwa wakati ulioelekezwa na Serikali, Jiji linatarajia kuajiri vijana wasiopungua 100 wenye sifa ikiwemo ya elimu ya kidato cha nne, wataalam wa kutumia kompyuta na wale wenye uwezo wa usomaji wa ramani ambapo watafanya kazi hiyo kwa siku 45” alisema Nkuba.
Aidha, mratibu huyo ametoa tahadhari kwa wananchi kutolihusisha zoezi hilo la uwekaji wa anuani za makazi na upimaji wa viwanja, badala yake wawe na ushirikiano kwa serikali kwenye zoezi hilo ili liweze kukamilika kwa wakati, na kwamba hilo ni zoezi la kitaifa na linafanyika katika kila Halmashauri hapa nchini.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.