MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule leo Oktoba 30, 2023, amehudhuria hafla ya utekelezaji wa Mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya Miji Tanzania ikihusisha ushindani (TACTIC) kwa Mkoa wa Dodoma unaotekelezwa na Kampuni ya CHINA GEO ENGINEERING CORP chini ya Mhandisi Msimamizi HONG - IK CONSULTANT CO. LTD kwa kushirikiana na GAUZE- PRO CONSULT (T) LTD na G & Y ENGINEERING CONSULT PLC hafla ambayo imefanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mradi huo unaotekelezwa na Serikali kuu chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia, una lengo la kuboresha miundombinu ya Barabara, madaraja, mitaro, majengo mbalimbali, vivuko vya barabara n.k pia una lengo la kujengeana uwezo kwa Taasisi tofauti tofauti.
Akizungumzia wakati wa hafla hiyo, Mhe. Senyamule amesema Dodoma ina hadhi ya Miji ya Kimataifa kutokana na vipimo vya hadhi hiyo hivyo miradi hii izingatie hadhi ya Jiji hili.
"Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ana maono na utashi mkubwa kwa Dodoma hivyo tunataka Jiji la Dodoma kuwa na hadhi ya Kimataifa kwani Mkoa huu umepimwa kwa asilimia 80 lakini tunataka kufikia asilimia 100. Dodoma haifananishwi na majiji mengine bali Miji mikubwa ulimwenguni hivyo, miradi hii ijengwe kwa hadhi hiyo na ubora huo wa Kimataifa. Nataka Mradi huu uwe moja ya miradi tunayopata taarifa yake kila mwezi" Mhe. Senyamule.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir Shekimweri, amesisitiza uzalendo kwa wasimamizi wa mradi huu pia matumizi mazuri ya fedha kwani zinatoka moja kwa moja kutoka Benki ya Dunia.
"Mradi huu si wa Jiji pekee Bali na wadau ambao ni Taasisi za miundombinu. Hatuhitaji ucheleweshwaji wa kukamilika kwake kwani mradi unasimamiwa na Jiji lakini fedha inatoka Benki ya Dunia hivyo kusiwepo na minong'ono ya fulani anakula fedha kwani hakuna ambaye itapita mikononi mwake. Tutangulize uzalendo kwenye hii kazi, tunataka tuone thamani ya fedha na kukamilika kwa mradi kwa wakati" Mhe. Shekimweri
Aidha, Mbunge wa Jiji la Dodoma Mhe. Anthony Mavunde amebainisha kuwa Dodoma ni kati ya mikoa inayoongoza kwa kuwa na mtandao mrefu wa barabara unaofikia takribani Km 70 hivyo miradi hii itasaidia kuliboresha Jiji la Dodoma kwa hadhi yake ya Makao makuu ya nchi. Pia amesema, miradi hii inakwenda kuboresha upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii. Ametoa Rai kwa viongozi kusimamia miradi hii kwa dhati ili wananchi waweze kushuhudia matokeo yake.
Mradi wa TACTIC ulisainiwa mara ya kwanza tarehe 13 Septemba 2023 chini ya Waziri wa TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa ambapo unahusisha ujenzi wa miundombinu kwa awamu tatu ambapo awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa masoko, mitaro, vivuko, stendi za mabasi, n.k na mpaka sasa maeneo yote yatakayojengwa chini ya Mradi huu yameshafanyiwa usanifu na tayari mkandarasi yupo katika hatua ya maandalizi kwa kufikisha vifaa kwenye eneo la ujenzi . Mradi unagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 24 bila Kodi ya ongezeko la thamani ( VAT) na unatarajiwa kutumia kipindi cha miezi 15
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.