SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Kongwa, Mhe. Job Ndugai ameshiriki uzinduzi wa Jengo la Mahakama ya Mwanzo Kibaigwa Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma leo Octoba 7, 2021.
Akizungumza katika uzinduzi huo Spika Ndugai alihimiza kituo hicho kitoe haki na kuwaomba viongozi wa wadini kusisitiza suala la haki katika sehemu zao.
"Nchi ikikosa haki basi imekosa kuwa karibu na Mungu" alisema Spika Ndugai.
Aliongezea kuwa haki ikicheleweshwa ni kama imekosekana, hivyo Mahakama inatakiwa kutekeleza haki zote ili haki hizo zionekane na kupatikana.
Aidha, alikemea ukatili wa kijinsia na kutaka uachwe mara moja hasa kwa wamama wajane wanaokosa haki zao au kucheleweshewa.
Alimalizia "sisi Bunge tunauheshimu muhimili wa Mahakama na tutaendelea kuwapa kila aina ya ushirikiano katika kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao."
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe. Najma Giga alisema kamati itaendelea kudumisha uhusiano mzuri na Mahakama ya Tanzania.
"Naipongeza Mahakama kwa miundombinu na teknolojia ya mawasiliano kwa kupiga hatua kubwa wanastahili pongezi", alisema Mwenyekiti Giga
Aidha, aliishuruku Mahakama kwa majengo mengi na mazuri yanayoendana na kiasi cha fedha kilichotumika.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Kitaifa akiwemo Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel, Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Prof. Sifuni Mchome, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya katiba na Sheria, Bw. Amon Mpanju, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Mustapher Siyani na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Remedius Mwema.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.