MWENGE wa Uhuru mwaka 2019 umezindua mradi wa Mtandao wa mabomba ya kusambazia maji safi kwenye mtaa wa Kinyambwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kuwahakikishia wananchi uhakika wa maji safi na salama.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Mzee Mkongea Ali baada ya kukagua na kuzindua Mtandao wa mabomba ya kusambazia maji safi eneo la Kinyambwa ’Extension’ wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani Dodoma mjini, alisema kuwa serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuhakikisha tatizo la maji linakuwa historia nchini kwa kusogeza huduma hiyo karibu na wananchi. Serikali itaendelea kujenga miundombinu ya maji ili kuboresha upatikanaji wa maji.
Awali akiwasilisha taarifa ya mradi wa ujenzi wa mtandao wa mabomba ya kusambazia maji safi eneo la Kinyambwa ’Extension’, Mhandisi David Pallangyo alisema kuwa mradi huo wenye mabomba yenye urefu wa kilometa 5.34 umetekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira mjini Dodoma (DUWASA). “Lengo kuu la mradi huu ni kufikisha huduma ya majisafi kwa wakazi wa eneo la Kinyambwa Extension, huduma ambayo itachochea shughuli za kijamii, ujenzi na uendelezwaji wa viwanja ambavyo tayari vimegawiwa kwa wananchi. Mabomba yaliyolazwa ni ya plastiki yenye vipenyo vya kati ya inchi 2 na inchi 6, alisema Mhandisi Palangyo.
Akiongelea utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi huyo alisema kuwa sehemu kubwa ya kazi ya ujenzi wa mtandao wa mabomba ya kusambazia maji eneo hilo ilifanywa na mamlaka yake kwa gharama ya shilingi 103,893,668. “Sehemu ndogo ya kazi ya kuchimba na kufukia mtaro, ujenzi wa chemba na ujenzi wa alama za njia ya bomba imefanywa na Mkandarasi Kampuni ya M/S. BAHAJ Construction Works. Kazi za ujenzi wa mtandao wa mabomba eneo hili ilianza 23/03/2019 na kukamilika 31/05/2019” alisema Mhandisi Palangyo.
Mradi huo umekamilika, na wateja 17 wameunganishiwa huduma ya maji wakati maombi 29 yamepokelewa kwa ajili ya kuunganishiwa huduma hiyo. Aidha, viwanja 1,743 vinatarajiwa kuunganishwa na huduma ya majisafi katika eneo hili, ambavyo ni sawa na jumla ya watu wapatao 10,458.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.