HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeanza kutekeleza mpango wa kutoa vibali vya ujenzi katika Kata zote 41 za Jiji hilo hususan kwenye maeneo ambayo yameshapimwa na kumilikishwa kwa ajili ujenzi wa makazi.
Hayo yamebainishwa na Msimamizi wa Uendelezaji katika Halmashauri hiyo Mhandisi Ally Bellah alipokuwa akizungumza na wakazi wa mtaa wa Chidachi Kata ya Ntyuka ambapo mkutano huo ulifanyika katika viwanja vya ofisi ya mtaa huo.
Bellah alisema tayari zoezi hilo limeshaanza kwenye Kata ya Mkonze na litachukua takribani wiki mbili kabla ya wataalam kupiga kambi katika Kata hiyo ya Ntyuka ambapo vibali vya ujenzi vitakuwa vinatolewa katika ofisi ya Kata na maombi yatafanyika hapo.
"Zoezi hili litafanyika katika Kata zote zenye maeneo yaliyopimwa na kumilikishwa pamoja na maeneo ambapo wananchi wamejenga bila vibali vya ujenzi kutoka katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ambayo ndiyo mamlaka ya upangaji, upimaji, na umilikishaji wa ardhi" alisema Bellah.
Mhandisi huyo alitoa wito kwa wakazi wa Dodoma hususan wale wenye nia ya kuanza ujenzi mpya kuhakikisha kuwa wanaomba kibali cha ujenzi kwanza ili kuepuka usumbufu na hasara ya kubomolewa jengo kwa kukwepa sheria na utaratibu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.