MRADI wa Kizazi Kipya uliokuwa unatekelezwa katika jiji la Dodoma kuanzia mwaka 2016 umewanufaisha watoto, vijana na walezi wanaoishi katika mazingira hatarishi kwa kusaidia huduma za afya ikiwemo VVU na UKIMWI, elimu, lishe na kuboresha kipato cha kaya.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa shirika la Action for Community Care – ACC, Pendo Maiseli wakati akizungumzia mradi huo katika mkutano wa kufunga mradi uliofanyika katika ukumbi wa Dodoma Hotel.
Mkurugenzi Maiseli alisema mradi wa Kizazi Kipya ulijikita zaidi katika kusaidia watoto na vijana wanaoishi katika mazingira hatarishi pamoja na familia zao kwa lengo la kuwapatia huduma muhimu na kuboresha maisha yao.
“Watoto na vijana waliofikiwa ni wale wanaoishi majumbani ambao walikuwa wanahudumiwa na shirika la Action for Community Care, na wale wanaoishi na kufanya kazi mitaani wakihudumiwa na shirika la KISEDET” alisema Maiseli.
Akitoa ushuhuda wa namna alivyonufaika na mradi wa kizazi kipya, mnufaika Frank Mlewa alisema kuwa mradi huo umemsaidia kupata ujuzi wa ufundi kwa sababu alipelekwa kusoma ufundi katika chuo cha VETA. “Mradi umenikuta nikiwa mtaani, tulikuwa wengi ulitukusanya ukatuunganisha pamoja ukatupa elimu katika chuo cha ufundi na sasa ni fundi naweza kujitegemea na nimepanga kwa sasa najitegemea” alisema Mlewa.
Kwa upande wake mnufaika Chipegwa Jonas alielezea vile ambavyo mradi huo umeweza kumnufaisha kwa kugharamikia gharama za masomo na afya. “Walikuja wakampa mama mtaji, walikuwa wananihudumia vitu vya shule, nilipofaulu nikawataarifu na bado wanaendelea kunisomesha” alisema Jonas.
Mradi wa kizazi kipya ulianza mwaka 2016 na umehudumia jumla ya watoto, vijana na walezi takribani 16,000 na unatarajiwa kuisha Septemba 2021 ukisimamiwa na kutekelezwa na mashirika ya Action for Community Care (ACC) na KISEDET ambayo yanapokea fedha kutoka Pact Tanzania.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.