HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma kupitia Idara ya Kilimo imeainisha vijana 100 ambapo kati yao vijana 20 wenye uzoefu wa ufundi wa ujenzi wa nyumba, useremala au uchomeleaji wamepatiwa mafunzo ya kujenga Kitalu Nyumba (Green House) ili kuwapatia ujuzi na kutumia fursa ya kilimo hicho ikiwa ni juhudi za kuongeza ajira kwa vijana.
Mafunzo hayo yametolewa katika eneo la Viwanja vya Maonyesho ya Kilimo Nanenane katika Kata ya Nzuguni Jijini humo, ambapo vijana hao wanatoka katika Kata mbili za Nzuguni, Ihumwa, Msalato, Michese na Miyuji.
Vijana wengine 80 wataungana na wenzao 20 na kupatiwa mafunzo ya ulimaji wa mboga mboga kwa kutumia Kitalu Nyumba kuanzia Machi 4 hadi 8, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Yustina Munishi kuhusu mradi huo, baada ya mafunzo kwa vijana hao kutolewa na Kitalu Nyumba kujengwa, kitaunganishwa na mfumo wa umwagiliaji kwa njia ya matone kabla ya kazi ya uzalishaji kuanza.
“Vijana hawa wametoka kwenye Kata za Nzuguni na Ihumwa ambapo ni jirani na eneo la mradi (Uwanja wa Nanenane) ili kuwapunguzia gharama” alisema.
Kwa mujibu wa Ofisa huyo, kwa sasa ujenzi wa Kitalu nyumba tayari umekamilika na shughuli ya kuunganisha na kujaribu mfumo wa umwagiliaji kwa njia ya matone inaendelea.
Mafunzo hayo ni juhudi za Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu katika utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi Nchini ambapo katika mwaka wa fedha 2018/19 pamoja na shughuli nyingine za kukuza ujuzi, imepanga kuwezesha nguvu kazi ya Taifa, hususani kundi la vijana ili wapate ujuzi na stadi katika kilimo kwa kutumia teknolojia ya Kitalu Nyumba (Green house technology).
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.