VIJANA wametakiwa kujikita katika kilimo cha zao la zabibu katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ili waweze kunufaika na fursa ya viwanda vilivyopo kwa kuuza mchuzi wa zabibu na kujipatia kipato.
Ushauri huo ulitolewa na Rehema Daud mwakilishi wa kiwanda cha kutengeneza mvinyo cha Dane kilichopo Nkulabi nje kidogo ya Jiji la Dodoma alipokuwa akiongelea fursa za kilimo cha zabibu katika banda la Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika viwanja vya maonesho ya Nanenane Nzuguni jijini hapa.
Rehema alisema “tupo katika maonesho ya Nanenane kuonesha bidhaa ya mvinyo mwekundu unaotengenezwa na kiwanda cha kuzalisha mvinyo cha Dane Wine. Pia, tunazalisha mchuzi wa zabibu ambao husambazwa katika viwanda vingine. Tuna mashamba mengi ya zazibu katika eneo la Nkurabi hapa Dodoma. Bahati nzuri iliyopo Dodoma ni mkoa ambao zabibu inastawi mara mbili kwa mwaka”.
Kutokana na hali ya kilimo cha zabibu kuwa nzuri, ni vizuri vijana wengi wakajikita katika kilimo hicho kinachoonesha mafanikio makubwa na kunufaika na uwepo wa viwanda vya kutengeneza mvinyo kwa ajira na kuongeza kipato, aliongeza Rehema.
Akiongelea soko la mvinyo, alisema kuwa soko ni zuri kwa sababu mvinyo unapendwa na watu. Alisema kuwa mvinyo wa Tanzania pamoja na kufanya vizuri nchini, haufahamiki nje ya nchi kutokana na kutokuutangaza.
Rehema Daud akaionesha bidhaa zinazozalishwa na kiwanda cha kutengeneza mvinyo cha Dane kilichopo Nkulabi nje kidogo ya Jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.