Na. Dennis Gondwe, DODOMA
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imewataka vijana kujiunga katika vikundi vinavyojishughulisha na kilimo cha zabibu ili waweze kupata mikopo ya halmashauri kwa ajili ya kuendeleza kilimo hicho.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru alipokuwa akitoa neno la kumkaribisha mgeni rasmi katika hafla ya utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika bustani ya Nyerere jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mafuru alisema “kuna shughuli za kilimo hazijasikika sana, lakini Mpunguzi na Hombolo kuna kilimo kikubwa sana cha zabibu na kuna vijana wanapambana wenyewe kwenye mapambano yao ya kilimo. Wakiwa na vikundi waje wapate mkopo. Sisi jiji la Dodoma, hatuogopi kumpa mtu milioni 300, milioni 400, hadi milioni 500 hata kama ni kikundi kimoja. Tunaweza kufanya kikao kimoja tu hapa cha kukipa kikundi shilingi milioni 800”.
“Sisi hapa hatuna ndugu, hatuna rafiki, hatuna tunayembeba. Wote wa Dodoma ni wa kwetu. Tunaingia mitaani kukusanya mapato kuhakikisha Dodoma inapaa. Nendeni kwenye ofisi za kata kuna maafisa maendeleo ya jamii wa kata, nenda kaeleze una shughuli gani na mna kikundi gani na taratibu gani za kupata fedha. Kimsingi kila robo ya mwaka Mheshimiwa mgeni rasmi huwa tunatoa shilingi Bilioni 1.2 hadi bilioni 1.4” alisema Mkurugenzi Mafuru kwa kujiamini.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.