Na: Hellen M. Minja
Habari - DODOMA RS
Mradi wa AHADI unaotekelezwa na Shirika la Kimataifa la 'World Vision Tanzania' kwa ushirikiano na Taasisi ya Tanzania Home Economics Association (TAHEA) unatajwa kuwanufaisha vijana rika balehe 13,218 wa Mkoa wa Dodoma kwa kuwafikia kwa elimu ya afya ya uzazi, kupinga ukatili wa kijinsia na stadi za maisha.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma CPA. Eric Ntikahera ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi Seksheni ya Usimamizi, Ufuatiliaji na Ukaguzi wakati wa kikao cha uzinduzi wa mbinu ya uwezeshaji jamii katika utoaji wa elimu ya ukatili wa kijnsia kupitia viongozi wa madhehebu ya dini kilichofanyika katika ukumbi wa Mesuma Jijini Dodoma Julai 23, 2025.
“Mradi wa AHADI kwa kipindi cha miaka mitatu umekua na manufaa makubwa katika Mkoa wa Dodoma kwa kuwafikia kwa elimu ya afya ya uzazi, elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia na stadi za maisha jumla ya vijana rika balehe 13,218 ambapo 2,639 ni wale walio nje ya shule (Ke-1,394 na Me-1,245) huku 10,579 (Ke-5504 na Me- 5,066) wakiwa katika shule 20 za msingi na sekondari”.
Aidha, Mkurugenzi Mwandamizi wa World VisionTanzania Dr. Joseph Mayalla, amesema katika kipindi alichotumikia Shirika hilo, ameona mabadiliko chanya pale ambapo viongozi wa dini walipopewa nafasi ya kushiriki katika utekelezaji wa Mradi huu kwani wanatoa huduma mbalimbali kupitia nyumba zao za ibada ambazo huleta matokeo kwa haraka.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa TAHEA, Bw. Peter Mapunda kutoka Taasisi hiyo amesema Mradi huo umefanikiwa kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana 409 kutoka Kata 10, vikundi vya vijana 138 vilifikiwa kwa elimu ya ujasiriamali, elimu ya utekelezaji wa bustani kwa vijana 363 wanaojiandaa kuingia kwenye malezi ya familia pamoja na vijana 2,639 waliunganishwa na kupatiwa huduma mbalimbali za afya.
Nae Bw. Kasei Msuya kutoka World Vision Tanzania, amesema mradi unalenga pia kuwafikia wazazi zaidi ya 274,000 na Viongozi wa madhehebu ya dini zaidi ya 2,110 waliopo Dar es Salaam na Dodoma hivyo, baada ya kikao hicho, viongozi hao watakua na jukumu la kufikisha taarifa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.