Ni Jambo la kawaida, unapokuwa unatembea mitaani katika nchi za Afrika kukutana na wachuuzi wa mtaani al maarufu wamachinga, kutokana na ukosefu wa ajira, lakini Alexanda Manyika na Noah Jotum ni wamachinga wanaobadili mtizamo wa kawaida kuhusu wachuuzi hao.
Mara nyingi, muonekano wa vijana hawa unakuwa sio wa kupendeza sana wala kuvutia kutokana na mavazi yao, hivyo kutowavutia wateja.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo, baadhi wa wachuuzi wameanza kuona umuhimu wa kazi yao hivyo kubuni njia mbalimbali za kuvutia wateja, ikiwemo kuvaa vizuri na kuwa watanashati.
Miongoni mwao, ni Alexanda Manyika na Noah Jotum ambao wote ni wachuuzi kutoka Mkoani Dodoma, nchini Tanzania, hawa ni vijana ambao wamekuwa wakiuza manukato mitaani kwa takriban miaka mitano sasa.
Mwanzo ukiwaona utadhani ni mapacha, vimo vyao vinafanana lakini zaidi pia unaweza kuwaweka katika kundi la wasanii chipukizi kutokana na mavazi yao ya kufanana. Wamejijengea umaarufu kutokana na utanashati wao ambao umekuwa ni gumzo mitaani.
"Unajua biashara ni ubunifu," Alexanda aliiambia BBC jijini Dodoma huku akiwa amebeba mfuko wake wa manukato na kujawa na bashaha. "Na lengo la kuvaa hivi ni sehemu ya ubunifu wetu. Huu umekuwa ni utambulisho na imetufanya tuwe tofauti na wengine. Ni kutokana na mavazi yetu mtu anaweza kusimamisha gari na kuuliza kuna nini," aliongeza.
Alexandar ndiye mwanzilishi wa ubunifu huo na baadae aliamua kupanua wigo kwa kumwingiza Noah katika biashara hiyo, na hivi sasa wanafanya kazi kama washirika.
Noah ana umri wa miaka mitatu tangu aingie katika biashara hiyo na anasema watu wanavutiwa sana na mtindo wao wa mavazi. "Kwa jinsi tunavyovaa, watu wanavutiwa sana na sisi, na hivyo kuongeza mapato, pia wateja wameanza kutuamini kwa muonekano wetu mbele ya watu," anasema Noah.
Je kuna uwiano wowote kati ya mavazi na faida wanayoipata? Alexanda anasema bei ya mavazi yao sio ya kutisha, bali ni bei za kawaida, ila kinachofanyika kikubwa ni ubunifu.
"Naweza kuchukua koti la kawaida, nikaliongezea ubunifu hapa na pale, na baadae likatoka tofauti kabisa. Sio gharama. Tunafahamu ili tuendelee lazima tujibane kwenye matumizi, na haya mavazi hayatuumizi," anasema Alexanda.
Vijana wengi ambao hawana ajira aidha wameshindwa kuona fursa ya kujiajiri kupitia umachinga au wamekuwa wakidharau kazi hii kwa kuhisi kipato chake ni kidogo. Hata hivyo, Alexanda na Noah ni miongoni mwa vijana wanaojivunia kwa mafanikio waliyoyapata kupitia kazi ya uchuuzi.
"Niseme tu wazi bila kificho. Kazi hii imenisaidia sana. Kwanza mbali na kipato, imenisaidia pia kimawazo, hata kukua pia kifikra, kuongeza ujasiri zaidi, hata kuongea mbele za watu, lakini tukirudi kwenye eneo la uchumi ambalo ndio lengo zaidi, biashara hii imenisaidia kuweza kulipia makazi yangu mwenyewe, lakini pia mavazi, kujilisha, lakini pia nimeweza kusomesha wadogo zangu na kuwasaidia wazazi wangu katika shida zao mbalimbali," anasema Alexanda.
Wateja wanaonekana kuvutiwa na muonekano wa Alexanda na Noah.
Amina Njogolo, ambae ni mteja anasema, "Ninapohudumiwa na watu wa aina hii ambao wapo smati kwanza najisikia vizuri na pia inanipa hali ya kuwaamini tofauti na vijana wengine ambao sio watanashati unaweza kuwadhania pengine waizi."
Nae Abdallah Twaha, anasema katika biasha ubunifu ni muhimu na hasa suala la utanashati kwa sababu wateja wanapenda kuhudumiwa na watu wasafi na wanaovutia.
Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika mashariki zinazokabiliwa na wimbi kubwa la ukosefu wa ajira kwa vijana wanaohitimu katika vyuo mbambali vya elimu ya juu na standi za ufundi. Mpaka sasa mkazo mkubwa umewekwa katika ujasiriamali ambapo ndipo kulipo na fursa za watu kujiajiri.
Chanzo: bbcswahili
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.