KIONGOZI wa Mbio za Mwenge maalum wa Uhuru kitaifa mwaka 2021, Lt. Josephine Mwambashi amekipongeza kikundi cha vijana cha Dodoma Data Tech TEHAMA na Umeme kwa uamuzi wao wa kujiunga na kujiajiri.
Pongezi hizo alizitoa wakati Mwenge maalum wa Uhuru mwaka 2012 ulipotembelea ofisi za kikundi hicho zilizopo Mtaa wa CDA jijini Dodoma.
Lt. Mwambashi alikipongeza kikundi hicho kwa kazi kinazofanya. “Kama vijana 10 wangeamua kuingia mtaani na kufanya uhalifu au wizi ni idadi kubwa, ila hawa wameamua kuungana kujiajiri. Niwapongeze Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuwapatia mtaji vijana hawa. Pia inawezekana kwa vijana kujiunga pamoja na kuanzisha mradi mkiwa na mtaji kidogo. Hii inawezekana, baada ya kuanza wadau wengine wataunga mkono” alisema Lt. Mwambashi.
Ni ukweli usiopingika kuwa serikali haiwezi kuajiri watu wote, lazima kuweke juhudi za kujiajiri wenyewe, alisema na kuwapongeza vijana hao.
Akiwasilisha taarifa ya kikundi hicho, Katibu wa kikundi, Efrem Mwalwebe alisema kuwa kikundi hicho kinaundwa na vijana 10, na kilianza mwaka 2020. Alisema kuwa kikundi kinajishughulisha na masuala ya TEHAMA na Umeme katika nyanja za ufundi. “Kikundi kilikuwa na kusajili kampuni tarehe 30 Machi, 2021 ambapo wazo lilitokana na changamoto katika upatikanaji wa kazi kubwa kwa kuwa kampuni inaaminika zaidi kuliko kikundi. Kikundi kiliomba mkopo na kufanikiwa kupata fedha kiasi cha shilingi 40,000,000 kutoka asilimia nne ya mkopo wa vijana unaotolewa na halmashauri” alisema Mwalwebe.
Kuhusu lengo la mkopo, alisema kuwa mkopo ulilenga kukiwezesha kikundi kupata vifaa vya kazi, ofisi na usafiri. Malengo mengine ni kushawishi matumizi ya mifumo ya TEHAMA na hatimae kujikwamua kiuchumi. Lengo lingine alilitaja kuwa ni kuisaidia serikali kupunguza tatizo la ajira kwa kutoa fursa za ajira kwa vijana wengine.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alimshukuru Kiongozi wa Mwenge maalum wa Uhuru kitaifa kwa kuridhia kazi zinazofanywa na kikundi hicho. Aidha, aliwashukuru wananchi waliojitokeza kwa wingi kuushangilia Mwenge maalum wa Uhuru mwaka 2021 wilayani Dodoma.
Mwenge maalum wa Uhuru mwaka 2021 unaongozwa na kaulimbiu isemayo “TEHAMA ni msingi wa Taifa endelevu; itumie kwa usahihi na uwajibikaji”
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.