Na Sifa Stanley, DODOMA.
VIJANA wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wameaswa kuwa waaminifu katika urejeshaji wa mikopo wanayopatiwa ili waendelee kunufaika na mikopo nafuu inayotolewa na Serikali.
Hayo yalisemwa na Mkuu Wa Idara ya Maendeleo ya Jamii na Vijana, Asha Vuai alipokuwa akitoa ufafanuzi wa suala la mikopo kwa vijana wakati wa mkutano wa afua ya afya ya uzazi na maendeleo ya vijana uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma uliohusisha mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali.
Vuai alisema kuwa, vijana lazima wajitambue na waoneshe uaminifu ili wapatiwe mikopo na serikali, ambapo uaminifu huo wanapaswa wauoneshe kwa kufanya miradi ya maendeleo kupitia fedha hizo pamoja na kurejesha mikopo waliyopatiwa kwa wakati.
“Vijana hawajitambui na hawatambui kuwa serikali ina lengo la kuwasaidia kujikwamua kiuchumi, inabidi wawe waaminifu ili mikopo iwe yenye manufaa” alisema Vuai.
Naye Afisa Vijana wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Manyama Mufungo alisema kuwa Serikali imejizatiti kuwakwamua vijana kiuchumi lakini bado kuna changamoto kwa baadhi ya vikundi vya vijana katika urejeshaji wa mikopo na wengine kutokuwa na elimu ya biashara na miradi yakuanzisha baada ya kupatiwa mikopo.
“Vijana hawana uelewa wakutosha kuhusu mikopo hii, unakuta kijana anakuja na kusema mimi nataka nipatiwe basi ama kikundi kinakuja na kusema sisi tunataka tupatiwe fedha tuchimbe kisima miradi inayogharimu fedha nyingi, wanasema hayo bila hata yakufanya tathimini ya mradi wao, pia baadhi vijana siyo waaminifu kurejesha mikopo” alisema Mufungo.
Aidha, Mratibu wa Afya ya Uzazi na Vijana, Fidei Obimbo alisema kuwa vijana wanapaswa kupatiwa elimu ihusuyo afya ya akili ili waweze kupata uelewa wa umuhimu wa urejeshaji wa mikopo hiyo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.