VIJANA waliopo katika mafunzo ya Kilimo chini ya Programu ya Building A Better Tomorrow (BBT) katika kituo cha Mafunzo cha Bihawana-Dodoma wameishukuru serikali chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuja na program hii ya BBT ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika kuwaongezea maarifa juu ya kilimo Biashara na hivyo kuwaandaa kuja kushiriki kikamilifu katika sekta ya kilimo.
Hayo yamesemwa na Kiongozi wa Vijana hao Ndg. Razack Mbaraka wakati wa ziara ya Naibu waziri wa Kilimo Mh. Anthony Mavunde kutembelea kituoni hapo na kujionea mafunzo yanayoendelea kwa vijana hao.
“Tunamshukuru Mh Rais Samia Suluhu Hassan na Wizara ya Kilimo chini ya uongozi wa Mh. Hussein M. Bashe kwa fursa hii ya mafunzo ya kilimo na kumilikishwa ardhi kwa vijana kupitia programu hii ya BBT.
Tangu tumejiunga hapa tumejifunza mambo mengi na kuongeza ujuzi mkubwa kwenye eneo la kilimo biashara, ni ahadi yetu kwamba kupitia mafunzo haya tutasaidia kuchochea ukuaji wa sekta ya kilimo kwa kulima kitaalamu na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya kilimo” Alisema Mbaraka.
Naye Naibu Waziri wa Kilimo Mh. Anthony Mavunde amewataka vijana hao kutumia fursa hiyo adhimu waliyoipata kwa kuchochea kuleta mageuzi kwenye sekta ya kilimo na kushawishi vijana wengi zaidi kushiriki kwenye sekta ya kilimo ili kundi hili kubwa la vijana litoe mchango kwenye kukuza sekta ya kilimo nchini na kuahidi kwamba serikali itaendelea kuhakikisha inaboresha mafunzo haya ya vijana ili kuwaandaa vyema vijana katika utelekezaji wa malengo ya Ajenda 10/30.
Akitoa maelezo ya awali Mratibu wa Programu ya BBT chini ya Wizara ya Kilimo Bi. Vumilia Zinkankuba amesema programu hii ya mafunzo inaendelea katika vituo 13 katika maeneo mbalimbali ya Tanzania na kwa sasa ipo hatua za mwisho na mafunzo hayo ya darasani na shambani na baada ya kukamilika kwake vijana watapelekwa mashambani kuanza uzalishaji wa mazao kwa vitendo.
Naibu waziri wa Kilimo Mh. Anthony Mavunde katika picha ya pamoja na vijana waliopo katika mafunzo ya Kilimo chini ya Programu ya Building A Better Tomorrow (BBT) katika kituo cha Mafunzo cha Bihawana-Dodoma alipofanya ziara na kutembelea kituoni hapo kujionea mafunzo yanayoendelea kwa vijana hao.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.