SHUGHULI za ubunifu na ukuzaji wa talanta ni njia sahihi ya kujiajiri vijana na kuweza kujitegemea na kukuza uchumi wao na taifa na kuepuka na utegemezi.
Kauli hiyo ilitolewa na mbunifu Dorothea Msigwa wakati akielezea fursa za ubunifu kwa vijana katika banda la Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP) katika maonesho ya kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu yanayoendelea katika uwanja wa jamhuri jijini Dodoma.
Msigwa alisema kuwa katika kipindi ambacho tatizo la ajira ni kubwa vijana wanatakiwa kufikiria njia mbadala ya kujiajiri. “Kwa vijana wote nawashauri tu talanta na ubunifu vinalipa. Umefika wakati kwa vijana kujituma katika kufanya kazi kwa sababu mwanzo wa kitu kimoja ndio njia ya mafanikio kwa kitu kingine, ndiyo imani yangu” alisema Msigwa.
Msigwa ambaye ni mwanafunzi wa Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini ni binti anayependa kazi za mikono. “Mimi nimebuni shughuli ninazofanya kwa mikono yangu. Ninatengeneza mapambo ya ukutani, ‘table mats’, maua ya urembo wa ndani na mazulia ya milangoni” alisema mbunifu huyo.
Alisema kuwa ubunifu wake unamsaidia kujiajiri mwenyewe na kuondoa tatizo la ajira. “Ubunifu wa kazi za mikono unanisaidia pia kuepukana na tamaa mbalimbali zinazotokana na masuala ya kiuchumi” alisema Msigwa.
Akiongelea soko la bidhaa zake, alisema kuwa soko lipo. “Soko ni kutokana na wewe mwenyewe muuzaji unavyo changamka kupata wateja. Kadri unavyojituma sana kutafuta wateja ndivyo soko linavyozidi kuwa kubwa. Jamii inayonizunguka inapendezwa sana na bidhaa zangu, si watoto, wakubwa hata wazee, kwa kifupi wao ndio wa kwanza kuniunga mkono” aliongeza Msigwa.
Mwanafunzi huyo mbunifu alikishukuru chou chake kwa msaada wa mawazo na maeneo ya kimkakati anaopata. “Chuo kimekuwa cha kwanza kutangaza bidhaa zangu kiujumla” alisema Msigwa.
Akiongelea jinsi ya kuweka mizania ya muda wa masomo na shughuli za ubunifu wa kazi za mikono anazofanya, alisema kuwa anajitahidi kuweka mizania sawa. “Kiukweli kila kitu na muda wake. Najitahidi sana kubana muda wa masomo na muda wa kufanya kazi zangu za ubunifu. Hivyo, muda wangu unakuwa umepangwakikamilifu.
Mwanafunzi huyo mbunifu alisema kuwa alipata mtaji wa kuanzisha shughuli zake za ubunifu kutokana na fedha za matumizi ya shule alizokuwa akipewa na mzazi. “Kwa mtaji wa kuanzia, kama nilivyo kueleza awali, napenda kazi za mikono hivyo, kwa kuwa mimi nasoma, mzazi alipokuwa akinitumia fedha ya matumizi nabakiza kama ya akiba na ndio mtaji wangu ukawa hivyo” alieleza kwa kujiamini.
Ikumbukwe kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaendesha Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) kwa madhumuni ya kutambua, kuadhimisha, kujenga, kukuza na kuendeleza ubunifu wa watanzania katika nyanja za sayansi na teknolojia ili kuchangia juhudi za kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa kati unaoendeshwa na viwanja.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.