Na; Happiness E. Chindiye
Habari - Dodoma RS
Vijana wameaswa kuondoa usiri na kutafuta maarifa kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo stadi za maisha na afya ya uzazi .
Hayo yamebainishwa na Afisa Elimu Mkoa wa Dodoma Mwl. Vicent Kayombo wakati akimwakilisha Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma kwenye ufunguzi wa semina ya kuwajengea uwezo Wanafunzi juu ya Stadi za Maisha na Afya ya Uzazi kutoka kwa wataalamu ambao walipelekwa kupata Mafunzi nchini Korea kwa ufadhili shirika la KOAT. Semina hiyo imefanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Jengo la Mkapa Julai 25,2025.
Mwl. Kayombo amesema lengo kuu la semina ni kujadili na shirika KOICA juu ya jambo muhimu sana linalohusiana na kuvunja ukimya au usiri kwenye maisha ya vijana wetu, ujuzi wa maisha, afya ya uzazi na hedhi salama kwa wote.
“Vijana tunapaswa kujitambua, kujua haki zetu, kujua miili yetu, na kujua namna ya kufanya maamuzi sahihi yanayolinda afya zetu. Tusiogope kuuliza maswali. Tusiogope kutafuta msaada kutoka kwa Wazazi, Walimu, au Wataalamu wa Afya.”-Ameeleza Mwl. Kayombo
Hata hivyo amewasihi wasimamizi na watekelezaji wa program hiyo kuwa na utu na uungwana kwa kuzingatia mila na desturi za Kitanzania , kwasababu inaweza kuwa upenyo wa kuziharibu mila zetu nzuri za Kitanzania kwani baadhi ya watu ambao sio waaminufu hutumia mwanya huo kupenyeza mafundisho mabaya kwa vijana ambayo yanawaangamiza wao na Taifa kwa ujumla.
Kwa Upande wake Mkurugenzi Mkazi wa KOICA Nchini Bw. Manshik Shin ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendeleza ushirikiano ,ambao utasaidia hasa Walimu kuongeza ujuzi wa Korea,na kuwa mabalozi wazuri kwa kuwa muda mwingi wanautumia kukaa na wanafunzi Shuleni.
Wafunzi kutoka katika Shule tatu za Mkoa wa Dodoma wamepata semina hiyo, ambapo wanatarajiwa kuwa Mabalozi kwa Wanafunzi wa shule nyingine za Mkoa huu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.