WAJASIRIAMALI jijini Dodoma wametakiwa kutumia fursa ya mikopo wanayoipata katika kuendeleza miradi yao ipasavyo sambamba na shughuli wanazotumia katika kuomba fedha hizo.
Wito huo umetolewa leo na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Jiji la Dodoma Sharifa Nabalang'anya katika mafunzo ya siku tatu kwa wajasiriamali juu ya matumizi sahihi ya mikopo yanayoendelea katika ukumbi wa shule ya Sekondari Umonga jijini hapa.
Mafunzo hayo ni mwendelezo wa elimu inayotolewa kwa wajasiriamali jijini hapa ikiwa ni hatua mojawapo ya kuwajengea uwezo katika kukabiliana na changamoto kubwa wanayokumbana nayo juu ya matumizi sahihi ya mikopo hiyo.
"Tunatoa mafunzo kwa vikundi 109 vya wajasiriamali wa makundi matatu ambayo ni vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kama sheria ilivyopitishwa na kuagiza Halmashauri zote Tanzania kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo kwa makundi haya.
"Tunatarajia kutoa shilingi milioni 853 kwa vikundi hivi, hivyo kabla hatujatoa fedha ni utaratibu wetu kuwapa mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi wa fedha, usimamizi wa miradi na namna ya kurejesha mikopo hii," alisema Nabalang'anya.
Pia amewasisitiza wajasiriamali jijini hapa kuhakikisha mafunzo wanayoyapata wanayatumia vyema ili waweze kujikwamua kiuchumi kuanzia ngazi ya familia na hata taifa kwa ujumla.
"Ujasiriamali unalipa na sasa hivi Dodoma ni jiji, tumieni fursa hii hakikisheni mnaongeza bidii katika shughuli mnazozifanya, pia hakikisheni mnajitangaza kupitia bidhaa mnazozalisha mkizingatia katika ubora wa kile mnachozalisha", alisema Afisa huyo.
Christopher Magesa ni moja kati ya wajasiriamali aliyepata mafunzo hayo, huku akisisitiza kuwa ataakuwa balozi mzuri kwa wengine katika kufikisha elimu hii kwa wajasiriamali ambao hawajapata mafunzo hayo.
"Nimejifunza mengi katika mafunzo hayo, yamenijengea uwezo wa kujiamini, nimepata pia kujua kwa kina kuhusiana na masuala ya mikopo na jinsi ya kuirejesha, kubwa zaidi nimefurahi kuwa na mikopo hii kutolewa bila riba ya aina yoyote," alisema Magesa.
Mafunzo hayo yamewakutananisha wajasiriamali jijini hapa na wataalam wa vitengo mbalimbali wakiwemo wataalam kutoka idara ya Mipango na Fedha, Mifugo, Kilimo na Ushirika katika kufanikisha wajasiriamali kufanya vitu walivyokusudia katika miradi yao kwa ufanisi zaidi.
Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Sharifa Nabalang'anya akiongea wakati wa mafunzo kwa wajasirimali wanaotarajiwa kukopeshwa mikopo isiyo na riba kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Wana vikundi wakisikiliza kwa makini maelekezo kuhusiana na matumizi bora na endelevu ya mikopo wakatayopewa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.