Na. Dennis Gondwe, IPAGALA
Vikundi na makampuni yaliyopewa dhamana ya kufanya usafi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma yametakiwa kujipanga na kuwajibika kufanya usafi katika maeneo yao kwa mujibu wa mikataba yao.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri katika maadhimisho ya siku ya Mazingira duniani leo tarehe 4 Juni, 2023 baada ya kushiriki zoezi la usafi wa Mazingira wa pamoja na wananchi wa Kata ya Ipagala jijini Dodoma.
Shekimweri alisema kuwa makampuni na vikundi vilivyopewa kazi ya kufanya usafi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma viwajibike kikamilifu kutekeleza majukumu yao. “Si vema tunafanya mazoezi ya usafi kama haya wakati kuna vikundi na makampuni ambayo tunayalipa kwa ajili ya kufanya usafi ila hayafanyi usafi huo kwa mujibu wa mkataba. Nataka kuona thamani ya fedha ikionekana. Halmashauri ya Jiji simamieni makampuni haya na vikundi hivi. Wakati mwingine muwakate mapato yao ili watekeleze majukumu yao vizuri. Natamani kuona magari ya usafi ni magari mazima. Siyo gari lenyewe na kuchukulia uchafu lenyewe linatembea na kuacha uchafu nyuma yake au kutoa harufu mbaya” alisema Shekimweri.
Aidha, aliwataka wakazi wa wilaya ya Dodoma kufanya suala la usafi kuwa tabia. “Usafi wa Mazingira iwe ni tabia yenu isiwe ni usafi kwa matukio kama haya ili kupiga picha za mitandao. Usafi ukiwa ni tabia yetu, mtu hatahitaji kuelekezwa, ataona ni wajibu kuishi katika Mazingira safi na salama. Nitoe rai kwa wafanyabiashara kufanya usafi katika maeneo yetu. Zaidi tuwe na vifaa vya kuhifadhia uchafu” alisema Shekimweri.
Aliwataka maafisa watendaji wa kata na mitaa kushirikiana na maafisa afya kukagua maeneo ili kubaini hali ya usafi. “Kwangu jambo hili ni changamoto lakini pia ni fursa, kuna sheria ndogo zitumieni kuongeza mapato. Mkikuta mazingira ni machafu pigeni faini” alisema.
Kwa upande wa Mkuu wa Kitengo cha usimamizi wa Usafi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro alisema kuwa halmashauri itaedelea kuhimiza wananchi kushiriki kufanya usafi wa Mazingira. “Jukumu letu ni kuhakikisha makao makuu ya nchi yanakuwa safi” alisema Kimaro.
Maadhimisho ya siku ya Mazingira yatafikia kilele chake tarehe 5 Juni, 2023, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika viunga vya Soko la wazi la Machinga jijini Dodoma chini ya kaulimbiu “Pinga uchafuzi wa Mazingira unaotokana na taka za plastiki”
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.