Na. Sifa Stanley, DODOMA
MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri amewaagiza Maafisa Afya wa Jiji la Dodoma kufanya ukaguzi katika Vilabu vya pombe ili kuhakikisha kuwa maeneo hayo kuna vifaa vya kunawa mikono na matundu yakutosha ya Vyoo.
Alitoa maagizo hayo katika maadhimisho ya siku ya unawaji mikono duniani ambayo kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma yalifanyika katika shule ya msingi Mtumba Kata ya Mtumba.
Akielezea faida za kunawa mikono kwa afya ya binadamu, Mkuu huyo alisema kunawa mikono kutaisaidia jamii kuepukana na magonjwa ya mlipuko na kuifanya jamii kuwa imara na yenye afya.
Ili kuhakikisha Wilaya ya Dodoma inajilinda na kujikinga na magonjwa ya mlipuko, Mkuu wa Wilaya aliagiza Maafisa Afya wa jiji la Dodoma kupita katika maeneo ya Vilabu vya pombe ili kukagua kama maeneo hayo wameweka vifaa vya kunawa mikono, na ikiwa hakuna vifaa vya kunawa mikono basi kilabu kifungwe mkapa watakapoweka vifaa hivyo.
“Nasisitiza kunawa mikono ukiingia msalani na nasisitiza kunawa mikono baada ya kutoka na kabla ya kujichanganya na jamii nyingine, lakini imekuwa ni kawaida sana ukitembea kwenye vichochoro na kwenye vilabu vya pombe unakuta mtu anaingi kichakani anajisaidia na humuoni akinawa mikono wala kujisafishisha kwa kutumia kitakasa mikono na narudi anajichanganya na jamii nyingine,
Sasa nielekeze ya kwamba hata katika vilabu vya pombe Maafisa Afya wa jiji letu wapite wahakikishe kuwa maeneo hayo kuna sehemu kwaajili ya kunawa mikono na ili wamiliki waendelee kufanya biashara ni lazima waweke maeneo ya kunawa mikono na matundu yakutosha ya vyoo, kwa kufanya hivyo nina imani tutapambana na magonjwa ya mlipuko”, alisisitiza Shekimweri.
Naye Msafiri Njani mkazi wa Kata ya Mtumba, aliuomba uongozi wa Kata ya Mtumba kuendelea kutoa elimu juu ya unawaji mikono ili kuinusuru jamii ya Mtumba dhidi ya magonjwa, lakini pia aliahidi kutoa hamasa ya unawaji mikono kwa vijana wenzake na wananchi wote kwa ujumla ili kuepuka magonjwa ya mlipuko.
“Mimi nitafata sheria na kanuni zote za unawaji mikono na nitaendelea kuwaelimisha vijana wenzangu kunawa mikono. Ungozi wa kata nawaomba wazidi kuhamasisha watu kunawa mikono kwasababu saivi kuna magonjwa mengi ya mlipuko ambayo ni hatari sana”, alisema Njani.
Naye Evelina Kusenha, mwanafunzi wa shule ya msingi Mtumba alielezea faida za kunawa mikono na kuwasisitiza wanafunzi wenzake kuendeleza desturi ya kunawa mikono wawapo shuleni na hata nyumbani ili kujilinda dhidi ya magonjwa.
“Kuna faida nyingi na umuhimu mkubwa wa kunawa mikono, kwasababu inasaidia kuepuka magonjwa kama vile kuhara na kuhara damu, pia kunawa mikono kunasaidia kuepuka magonjwa ya mfumo wa upumuaji, wanafunzi wenzangu tuendelee kunawa mikono kwa maji safi na sabuni”, alieleza Kusenha.
Ifikapo Oktoba 15 ya kila mwaka Dunia huadhimisha siku ya unawaji mikono Duniani, lengo likiwa ni kuendelea kujenga ulimwengu wenye afya na kusaidia kupigana vita dhidi ya magonjwa mbalimbali ya mlipuko.Katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma maadhimisho haya yalifanyika katika Shule ya Msingi Mtumba iliyopo Kata ya Mtumba yakiwa yamebeba kaulimbiu isemayo “Tuungane pamoja kuhakikisha usafi wa mikono kwa wote”
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.