MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri awaomba viongozi hususani wa ngazi ya wilaya wanapoenda kwenye ratiba za upandaji miti katika maeneo mbalimbali kuhakikisha wanapanda kitalu kizima na kukisimamia.
Hayo ameyasema jijini Dodoma kwenye hafla ya uzinduzi wa zoezi la upandaji miti katika eneo la Tambukareli ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar yatakayofanyika Januari 12 mwaka huu.
Shekimweri amesema kuwa viongozi ngazi ya wilaya katika Mkoa wa Dodoma wanapoenda kwenye ratiba ya upandaji miti waambatane na marafiki zao wapande kitalu kizima na kukisimamia ili kusudi, tija na dhana yakukijanisha Dodoma iweze kufikiwa.
“Aende Shekimweri na marafiki wa Shekimweri wasiishie kupanda mti mmoja na kuondoka bali wapande kitalu kizima na kukisimamia wakishirikiana na klabu za mazingira katika eneo husika,”alisema Shekimweri.
Akiongelea wiki ya maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar, Shekimweri alisema “Tunaadhimisha Mapinduzi matukufu kule Zanzibar, kama kuna Mapinduzi zaidi tunayahitaji ni haya yakukijanisha Dodoma. Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan akiwa Makamu wa Rais aliasisi kampeni ya Kijanisha Dodoma, Dhamira yetu nikukijanisha Dodoma na kuweka mandhari ya kuvutia lakini salama pia kuondoa ‘stress’ za maisha ya mjini. Nikuhakikishie kama ambavyo tumewasilisha kwenye mchoro tutashirikana na wadau mbalimbali kusimamia ili kusudi dira hiyo tuweze kuifikia”.
Alimalizia kwa kutoa shukrani kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira ), Dkt. Seleman Jafo. “Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ameniomba nikushukuru sana kwa namna ambavyo unashirikiana na Ofisi ya Mkoa katika agenda ya kukijanisha Dodoma, agenda ni kubwa na mahitaji ni makubwa yanataka maono mapana ya kisera nanikiri wizara yako na wewe mwenyewe mmekua na mchango mkubwa sana kwa Ofisi ya Mkoa na Wilaya” .
Mapinduzi ya Zanzibar yalitokea mwaka 1964 ili kumuondoa madarakani sultani wa Zanzibar na serikali yake iliyoundwa hasa na waarabu na hatimaye kuweka uongozi mikononi mwa waafrika ambao ndio wengi visiwani humo .
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.