Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi amewataka viongozi wapya waliochaguliwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa hivi karibuni kuachana na tabia ya kujali maslahi binafsi badala yake waende kutenda haki kwa wananchi waliowachagua na kwa kufanya hivyo kutawasaidia kuaminika kwa wananchi.
Kunambi ameyasema hayo jijini Dodoma katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Mipango jijini hapa, katika tukio la kuwaapisha viongozi wapya wa Serikali za Mitaa ambao walichaguliwa tarehe 24 Novemba, 2019.
Wakati huohuo, kunambi amesema watakuwa na utaratibu wa kutoa tuzo kwa mitaa kumi kila baada ya miezi sita katika Jiji la Dodoma. Alisema kuwa Jiji linahitaji kuwa na mfumo shirikishi kwa wananchi ili kila mwananchi katika Mtaa wake awe sehemu ya kusimamia sheria na taratibu zilizowekwa na Serikali.
Ninyi ni viongozi wapya, muende mkatumikie wananchi kwa haki. “Utatuzi wa migogoro ni jukumu lenu, usimamizi wa shughuli za maendeleo katika ngazi ya mtaa ni jukumu letu. Na hii ni kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara 145, inawapa hayo majukumu. Lakini pia sheria za Serikali za Mitaa, Mamlaka ya Miji, sura 288 inatupa hayo majukumu” alisema Kunambi.
Awali akitoa taarifa fupi ya mwenendo wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Jiji la Dodoma uliofanyika tarehe 24 Novemba 2019, Msimamizi wa uchaguzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro amesema kuwa mitaa yote katika Jiji la Dodoma iliweza kushiriki katika hatua za awali za uchaguzi. Vyama vilivyoshiriki uchaguzi huo vilikuwa ni Chama cha Mapinduzi (CCM), ACT Wazalendo, CHADEMA, Allience for African Farmers Party (AFP), Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Umma (CHAUMA) pamoja na Chama cha Demokrasia Makini.
Katika hatua nyingine Kimaro amesema kuwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mwaka huu ulisimamiwa na kuendeshwa kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa ngazi ya vijiji, vitongoji na mitaa za mwaka 2019. Miongozo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa iliyotolewa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI pia ilitumika, aliongeza.
Zoezi la kuwaapisha viongozi wa Serikali za Mitaa lilifanywa na Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Pascal Mayumba. Viapo viwili vilifanyika, kiapo cha uaminifu na kiapo cha utii na uadilifu
.Viongozi wa Serikali za Mitaa wa Jiji la Dodoma wakila kiapo cha utii leo, tayari kwa kuanza kutumikia vyadhifa zao mpya baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.