KATIKA kusisitiza amani na utulivu wakati wa kumalizia kampeni na kisha kupiga kura Oktoba 28, mwaka huu, viongozi wa dini wamewataka wananchi kujitokeza kupiga kura na mara wakipiga kura waende nyumbani kupumzika wasizagae mitaani.
Viongozi hao waliongea kwa nyakati tofauti katika mkutano wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dodoma jijini hapa jana wakinukuu vitabu vitakatifu vya Biblia na Korani, walisema kupiga kura ili kuchagua viongozi si haramu, hivyo kila kiongozi wa dini katika madhabahu na mimbari yake anatakiwa kwenda kuhamasisha waamini na waumini wake wenye sifa kwenda kupiga kura kwani hilo ni takwa la kikatiba na kidini pia.
Akiufungua Mkutano wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge aliwataka viongozi hao kutumia nafasi zao kuhubiri amani na utulivu na asiwepo mtu atakayetumia uchaguzi kuwa kigezo cha kuwagawa wananchi na ushindani usiweke rehani amani iliyodumu miaka mingi hapa nchini.
Mchungaji Kanisa la Calvary Assemblies of God Kisasa Relini jijini hapa, Visenti Malenda alisema ili kudumisha amani na utulivu baada ya kupiga kura Oktoba 28, 2020 wananchi wote wanatakiwa kuambiwa kuondoka vituoni na kwenda kupumzika nyumbani.
Mchungaji Malenda aliongeza kuwa inatakiwa kutolewe msisitizo wa kutoruhusu vijana kurandaranda na kuendeleza hoya hoya mitaani kunachangia kuwaingiza katika matatizo ambayo si ya lazima na hawastahili.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini mkoani Dodoma, Sheikh Mustaferpha Shaban alisema viongozi wa dini hivi karibuni wengine wamepotoka kwa kunadi sera, kutangaza wagombea na kushabikia vyama vya siasa kazi ambayo si wajibu wao.
Aliwataka viongozi wa dini kuacha kujiingiza katika masuala ya siasa na kuwaachia wanasiasa, wao kama viongozi wa dini wanatakiwa kuonya na kuonesha mema, “Kuingia katika jukwaa la kampeni na kunadi vyama, wagombea au kunadi sera za vyama si jukumu la viongozi wa dini,”
Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la Philadelpia Assembly of God, Dkt. Yohana Masinga alisema Taifa la Tanzania limempa nafasi Mungu na kiongozi wake akaamua kumpa Mungu nafasi wakati wa Corona, vile vile viongozi wa dini wanatakiwa kuomba ili Mungu uchaguzi upite salama.
Vilevile, Mjumbe wa Baraza la Masheikh Mkoa wa Dodoma Sheikh Kisusu Mvumbo alisema, amani inatakiwa kutamalaki nchini kwa kuhakikisha kwamba wao kama viongozi wa dini wanaombea uchaguzi unakuwa wa amani na utulivu.
Akichangia Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Dkt. Brown Mwakipesile alisema, Taifa la Tanzania linamhitaji Mungu wakati wa uchaguzi ili kupata viongozi watakaolivusha kwani kwa kumtegemea yeye kila jambo litawezekana na uchaguzi utakuwa wa amani.
Katibu wa Vijana katika Kanisa la Anglican mkoani Dodoma, Mchungaji Cosmasy Maginda alisema katika kuepusha malalamiko kila chama hata kama kidogo kinatakiwa kupewa haki mfano kila chama kinastahili kupata ulinzi wa kutosha hata kama kina wafuasi wachache hawana budi watendewe haki ya kupewa ulinzi.
Ndipo Askofu wa Kanisa la Mlima wa Moto mkoani Dodoma, Sylvanus Komba aliomba uongozi wa Vyama vya Siasa kuendelea kutoa elimu kwa viongozi mbalimbali wakiwamo wa dini wakati wote badala ya kungoja wakati wa uchaguzi tu, kwani ng’ombe hanenepi siku ya mnada.
Baadae, Afisa Tawala Mwandamizi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Prudensia Kwabila akasema, vyama vya siasa vizingatie sheria za nchi zikiwemo za uchaguzi na sheria ya gharama za uchaguzi, sheria za vyama vya saisa na kanuni zake ili kudumisha uhusiano mwema, utii wa sheria bila shuruti na uvumilivu wa kisiasa pamoja na amani na utulivu.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Josephat Maganga aliwataka viongozi wa dini kushikamana na viongozi wa serikali kuhakikisha katika mkoa wa Dodoma uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu ili kupata viongozi watakaoleta maendeleo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Maduka Kessy alisema, viongozi wa kanisa wakiwemo maaskofu, masheikh, wachungaji, maimamu na viongozi wengine wana nafasi ya kuivusha nchi kwa kuomba uchaguzi uwe wa amani, upendo na mshikamano.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge (wa pili kulia), Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoani Dodoma Sheik Mustaferpha Shabani (kulia), Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Josephat Maganga (kushoto) na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Maduka Kessy (wa pili kushoto) wakiwa katika meza kuu wakati wa kikao Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dodoma.
Baadhi ya viongozi wa Dini wakisilikila wakati kikao kikiendelea.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.