Na. Dennis Gondwe, DODOMA
VIONGOZI wa vyama vya siasa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kufanya kampeni za kistaarabu ili Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kufanyika kwa amani na utulivu.
Kauli hiyo ilitolewa na Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko alipokuwa akiongea na waandishi wa habari na wadau wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ofisini kwake leo wakati akiwaelezea mwenendo wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Dkt. Sagamiko alisema kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mujibu wa Kalenda ya Uchaguzi zinafanyika siku saba kabla ya tarehe ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Hivyo, kampeni zilianza jana tarehe 20 Novemba, 2024 baada ya vyama vya siasa kuwasilisha ratiba ya mikutano ya kampeni kwa Msimamizi wa Uchaguzi. Ratiba hizo zilishawasilishwa kwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Dodoma. Mkuu wa Polisi Wilaya anawajibu wa kuhakikisha ulinzi na usalama katika mikutano ya kampeni. Mikutano ya kampeni itaanza saa mbili asubuhi na itamalizika saa kumi na mbili kamili jioni ya kila siku ya kampeni”.
Akiongelea mabadiliko ya ratiba kwa vyama vya siasa pale inapobidi alisema kuwa yawasilishwe kwa maandishi. “Iwapo chama cha siasa chenye mgombea kitahitaji kufanya mabadiliko ya ratiba ya mikutano ya kampeni kitatakiwa kuwasilisha kwa maandishi mapendekezo ya mabadiliko hayo kwa Msimamizi wa Uchaguzi na mapendekezo hayo kuridhiwa kwa mujibu wa kanuni. Baada ya mapendekezo hayo kuridhiwa na vyama vya siasa yatawasilishwa kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya kwa ajili ya kupatiwa ulinzi kwenye mikutano ya kampeni” alisema Dkt. Sagamiko.
Msimamizi huyo wa uchaguzi alisema kuwa yapo masharti ya kampeni za uchaguzi ambayo wagombea na vyama vya siasa hawaruhusiwi kufanya katika mchakato wa uchaguzi. Masharti hayo yanalenga kuhakikisha kampeni zinafanyika kistaarabu na kudumisha amani na utulivu. “Kutoa maneno yanayolenga uvunjifu wa amani au kuchochea vurugu. Kutumia rushwa wakati wa uchaguzi, kutoa maneno ya kashfa na matusi na kutumia ubaguzi wa jinsia, dini na kabila” alisema Dkt. Sagamiko.
Aidha, aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kufuatilia na kusikiliza kampeni za vyama vya siasa ili kufahamu sera za wagombea mbalimbali. Kampeni za vyama vya siasa zitawasaidia kufanya maamuzi siku ya kupiga kura tarehe 27 Novemba, 2024, aliongeza.
MWISHO
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.