Marais Wastaafu pamoja na Mawaziri Wakuu Wastaafu wamefanya ziara ya siku moja kukagua Mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa – SGR kuanzia Kilosa mkoani Morogoro hadi jijini Dar es Salaam, leo Julai 06, 2021.
Marais Wastaafu walioshiriki ziara hiyo ni Rais wa awamu ya pili Mhe. Ali Hassan Mwinyi na Rais Mstaafu wa awamu ya Nne Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete wakiambatana na Mawaziri Wakuu Wastaafu Mhe. John Malecela na Mhe. Mizengo Peter Pinda pamoja na viongozi mbalimbali wakiwemo wakuu wa mikoa na Wilaya ambazo mradi wa SGR unapita katika maeneo yao.
Lengo la ziara hiyo ni kuona kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ambayo utekelezaji wake ni mipango iliyowekwa na Marais wa awamu zilizopita.
Marais hao waliweza kuona maendeleo ya mradi ambapo walitembelea handaki lenye urefu wa zaidi ya Kilometa moja lililopo Kilosa mkoani Morogoro, Stesheni za SGR za Morogoro, Ngerengere, Soga na kuhitimisha ziara yao katika jengo la Tanzanite ambalo ni Stesheni kuu ya SGR jijini Dar es Salaam.
Aidha, Waheshimiwa Viongozi Wastaafu hao wakiwa ndani ya treni ya Uhandisi inayomilikiwa na mkandarasi Yapi Merkezi walipata fursa ya kujionea kazi mbalimbali zikiendelea ambazo kwa kiasi kikubwa ni kazi za kuhitimisha Mradi huo kwa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro ambacho kimefikia zaidi ya asilimia 92.
Viongozi hao wastaafu walionesha kuridhishwa na kufurahishwa na jitihada za serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Samia kupitia Shirika la Reli Tanzani – TRC kwa utekelezaji na usimamizi wa mradi huo huku wakieleza faida ambazo nchi itazipata kupitia mradi huo katika nyanja ya Kijamii na kiuchumi.
“Tunamshukuru muasisi wa kazi hii Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwa fikra njema, kwani kila jambo linaanza na fikra, kafanya kazi nzuri pamoja na awamu ya sita ambayo Mhe. Samia Suluhu Hassan ameanza vizuri kwa kuendeleza yale ambayo walikuwa wanayafanya na mwenzie, pia namuombea aweze kuendelea kufanya yale mazuri waliyoanzisha” amesema Mhe. Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa awamu ya pili.
Rais Mstaafu wa awamu ya nne Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa amefurahishwa kuona mipango iliyopangwa na Marais waliotangulia inatekelezwa kwani mpango wa kujenga reli ulikuwepo tangu kipindi cha Hayati Benjamin William Mkapa, Rais wa awamu ya tatu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye aliweka mpango wa kujenga reli kwa kiwango cha kimataifa kutoka Dar es Salaam - Isaka hadi Kigali, Isaka – Mwanza, Tabora - Kigoma na Kaliua – Kalema.
“Jambo la faraja ni kwamba tunapata reli ya kisasa yenye uwezo wa kubeba mzigo mkubwa zaidi na abiria wengi, hili ni jambo la kufurahisha na kuwashukuru wote waliotoa wazo la kuwa na reli ya namna hii lakini kubwa zaidi ni kwa wale waliothubutu”
Mhe, Rais Mstaafu Kikwete aliongeza kuwa Mradi huu utasaidia kupunguza muda wa safari na kuongeza ufanisi katika ubebaji mizigo na abiria na kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi kwa kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi.
Mkurugenzi Mkuu wa TRC Masanja Kadogosa amewashukuru Viongozi hao Wastaafu kwa kutembelea Mradi wa SGR kwa kuwa usanifu wa mradi huo ulianza kipindi cha Hayati Benjamini Mkapa hivyo watanzania watarajie mambo mazuri kwani mradi huo unaendelea vizuri na hivi karibuni huduma zinatarajiwa kuanza kutolewa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.