ZOEZI la utoaji wa chanjo ya kinga dhidi ya ugonjwa wa Saratani ya Shingo ya Kizazi kwa Wanawake limezinduliwa rasmi katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma huku wasichana waliopatiwa chanjo hiyo wakitoa wito kwa wenzao kujitokeza na kuhakikisha wanakingwa dhidi ya ugonjwa huo.
Uzinduzi huo umefanyika jana katika ukumbi wa Dodoma Sekondari ambapo mgeni rasmi katika hafla fupi ya uzinduzi huo alikuwa Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Deo Ndejembi huku Mganga Mkuu wa Halmashauri Hamadi Nyembea akimwakilisha Mkurugenzi Godwin Kunambi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Kaimu Mkuu huyo wa Wilaya alisema uzinduzi huo ni kiashiria cha kuwafikia Wasichana wote wenye chini ya umri wa miaka 14 ndani ya Wilaya ya Dodoma.
Alisema zoezi hilo litaendeshwa na Halmashauri kupitia Ofisi ya Mganga Mkuu, na litashirikisha viongozi wa ngazi zote ikiwemo Kata na Mitaa ili kuhakikisha kila msichana anayehusika anafikiwa na kupatiwa chanjo hiyo.
Awali, Mganga Mkuu wa Halmashauri Hamadi Nyembea alisema katika kipindi cha Mwaka mmoja ujao, jumla ya Wasichana 7,828 walio na umri wa chini ya miaka 14 wanatarajiwa kufikiwa na kupatiwa chanjo hiyo katika Wilaya ya Dodoma.
Alisema baada ya miezi sita Wasichana wote waliopatiwa chanjo hiyo watapatiwa tena kwa awamu ya pili ili kukamilisha kinga yao dhidi ya virusi vinavyoeneza ugonjwa huo.
Alimweleza Mgeni rasmi na wajumbe kuwa, chanjo hiyo imethibitishwa na Shirika la AfyaDuniani (WHO) hivyo Wasichana na Wazazi wasiwe na mashaka badala yake watoe ushirikiano wa kutosha ili kufikia lengo la Serikali la kutokomeza ugonjwa huo kama ilivyofanya kwa magonjwa kama Polio.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.