WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema, wakimbizi na raia kutoka nje ya nchi wanapewa vitambulisho vya Taifa hivyo unahitajika umakini mkubwa kwa ajili ya usalama wa nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Kangi Lugola amesema leo kuwa, yeyote anayefanya kazi katika Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) anapaswa kuwa makini na ndiyo maana mamlaka hiyo ipo kwenye wizara hiyo kwa kuwa inafanya kazi za kiusalama.
“Uchakati wa taarifa za mtu binafsi ni suala la kiusalama, tunakwenda nalo kiumakini kuhakikisha kwamba mtu ambaye anatakiwa apewe hiki kitambulisho, kwa sababu tunawapa makundi matatu, tunampa mtu ambaye ni raia wa Tanzania, lakini tunampa mkimbizi, lakini pia tunampa mtu ambaye ni kutoka nje ya nchi, tunawapa hivi vitambulisho vitavyoitwa ni vya Taifa” amesema Lugola wakati akizungumza kwenye kipindi cha Asubuhi leo kinachorushwa na kituo cha redio cha TBC Taifa cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Waziri Lugolo amewaomba Watanzania waelewe kwamba, kuchelewa kupata namba za vitambulisho vya Taifa au vitambulisho vyenyewe si uzembe kwa kuwa kazi hiyo ni nyeti na inahitaji umakini.
“Na ndio maana kuna maneno mawili utambuzi yaani mtu atambuliwe kwanza halafu pia tumsajili halafu ndio tuweze kumhakiki na baadaye ndio tuweze kumpa sasa namba ya utambulisho kwamba huyu tumeridhika nae” amesema Waziri Lugola.
Amesema walipanga hadi Desemba mwaka huu NIDA iwe imesajili watu milioni 24.5 na hadi Novemba 13 takribani Watanzania milioni 20.5 walikuwa wamesajiliwa kwenye mfumo na kati ya hao tayari namba milioni 15.5 zimezalishwa.
“Tunakimbizana kuhakikisha kwamba lengo hilo la watu milioni 24.5, namba zao za utambulisho zitakuwa zimekwishazalishwa ifikapo tarehe 31 Desemba kwa hiyo namba zitakuwa zinatumika huku tukiendelea kuhakikisha sasa tunakamilisha kitambulisho chenyewe kiweze kufika kwa kila Mtanzania ambaye amebainishwa na tayari amesajiliwa na taarifa zake binafsi zipo kwenye kanzidata ya Taifa ambayo inamuhusu mwananchi mwenyewe”amesema Lugola.
Chanzo: habarileo.co.tz
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.