Na. Dennis Gondwe, DODOMA
SHULE ya sekondari Viwandani iliyopo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma imetakiwa kupandisha kiwango cha taaluma ili kiendane na hadhi ya kuwepo makao makuu ya nchi kwa kuwatengenezea wanafunzi mazingira bora ya kujifunzia na walimu mazingira bora ya kufundishia.
Agizo hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe alipoingoza kamati hiyo kutembelea na kukagua hali ya ujenzi na ukarabati wa vyumba vya madarasa na ujenzi wa uzio wa shule ya sekondari Viwandani jijini hapa.
Prof. Mwamfupe alisema kuwa kiwango cha taaluma hakiridhishi na kusadifu uwepo wa shule hiyo makao makuu ya nchi. “Shule hii ipo hapa usoni kabisa mwa Jiji, lazima mjitahidi kupandisha hali ya taaluma. Hatuwezi ongelea elimu bora wakati wanafunzi hawapo madarasani. Ndiyo maana tumejenga madarasa hapa ili wanafunzi wapate sehemu ya kusomea na kujadili ubora wa elimu tunayowapa. Mwalimu lazima uwe na takwimu zote muhimu za shule katika viganja vya mikono yako” alisema Prof. Mwamfupe.
Prof. Mwamfupe ambaye ni Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma aliushauri uongozi wa shule hiyo kupanda miti ya aina mbalimbali. “Umefika wakati wa shule kupanda miti ya kutosha shuleni hapa. Wekeni vimbwete ili wanafunzi wapate sehemu nzuri ya kujisomea nje ya madarasa. Vimbwete na kivuli cha miti vitasaidia kuboresha mazingira ya wanafunzi kujisomea na kupandisha ufaulu” alisema Prof. Mwamfupe.
Katika hatua nyingine, Meya huyo aliwashauri walimu wa shule hiyo kuanzisha umoja utakaokuwa kimbilio lao wakati mgumu. “Niwashauri kuanzisha umoja wenu hapa ili uweze kuwasitiri walimu mnapokumbana na changamoto, inaweza kuwa Saccos ya walimu” alisema Prof. Mwamfupe.
Akiwakaribisha wajumbe wa Kamati ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika Shule ya Sekondari Viwandani, Mchumi katika halmashauri hiyo, Abeid Msangi alisema kuwa Halmashauri ilipeleka shilingi 20,000,000 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vyumba vya madarasa na ujenzi wa uzio shuleni hapo.
Kamati ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilifanya ziara ya kikazi kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi iliyotekelezwa na jiji hilo kwa kipindi cha robo ya nne (Aprili-Juni, 2022).
Mhe. Sospeter (kushoto) akimsikiliza mwakilishi wa Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari Fredrick Mwakisambwe akitoa maelezo hali ya taaluma shuleni Viwandani.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.