Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo jana tarehe 6/8/2020) akiambatana na timu ya wataalam walitembelea kufanya ukaguzi wa mwisho wa viwanja ambavyo Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliahidi kutoa kwa wachezaji wa timu ya Taifa "Taifa Stars" ambayo ilifuzu na hatimaye kushiriki kwa mara ya kwanza baada ya miaka 40 michuano ya fainali za Afrika. Mwaka jana Mhe. Rais alitoa zawadi yake na alisema kwa niaba ya Watanzania ametoa zawadi kwa wachezaji wa timu, benchi la ufundi, vilevile alitoa zawadi hiyo kwa wachezaji wa zamani wa timu ya Taifa Peter Tino na Leodiger Tenga ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Tanzania ambao walikuwepo kwenye timu ile ya mara ya mwisho ya mwaka 1980 iliyoshiriki mashindano ya Afrika yaliyofanyika nchini Nigeria.
Akizungumza alipowakaribisha Ikulu wachezaji wa timu ya Taifa tarehe 25 Machi, 2019 kuwapongeza baada ya kuifunga timu ya Taifa ya Uganda mabao 3 - 0 na kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika, Rais alisema kilichofanywa na Taifa Stars pamoja na bondia Mwakinyo na mwalimu wake ameona kwa niaba ya Watanzania ameamua kutoa zawadi hiyo ya viwanja kwa wachezaji wote. "Sina chochote kikubwa cha kuwapa, ila nimeguswa na nimeona nitoe zawadi ndogo. Tutawapa viwanja vya kujenga nyumba. Wachezaji wote wa Taifa Stars , Hassan Mwakinyo, mwalimu wake, Peter Tino pamoja na Leordiga Tenga wote wapate viwanja. Viwanja hivi vitakuwa Dodoma ambako ndiko Makuu makuu ya nchi.
"Kila mmoja apate kiwanja chake, kama Serikali ilitoa viwanja kwa mabalozi wa nchi nyingine, hatuoni sababu ya mabaloz wa Taifa letu (Taifa Stars na Hassan) kwanini wasipatiwe viwanja. Haiwezekanani baada ya kustaafu wanabaki hawana kitu , lazima tutambue kazi ambayo wameifanya kwa niaba ya nchi yetu ," alisema Rais Magufuli.
Dkt. Abbas alielezea kuwa mchakato umeendelea na hatimaye umekamilika, huku akiwaonesha waandishi wa habari maeneo ambapo kumetengwa viwanja vya wachezaji wa timu ya Taifa na makocha akiwemo pia bondia Mwakinyo na kocha wake ambao pia walikuwepo kwenye orodha ya kupata.
"Ni eneo zuri, ni eneo la Mtumba hapa Makao Makuu Dodoma mbele kidogo ya Mji wa Serikali na nyumba kidogo ya kona ya kona ya kwenda barabara ya Ikulu ilipo ikulu ya Chamwino, na ni eneo ambalo lipo karibu na barabara kuu ya Dar es Salaam kuja Dodoma, ni kama umbali wa kati ya mita 250 mpaka 300 kutoka barabara kuu.
Kwa hiyo tumejiridhisha, viwanja hivi ni vikubwa ni eneo zuri na vina ukubwa wa kati ya mita za mraba 1,200 mpaka 2,300. Tunapokamilisha zoezi hili ambayo ilikuwa ni ahadi ya Mhe. Rais liwe pia chachu kwa vijana ambao wanashiriki michezo mbalimbali, lakini iwe chachu kwa vyama, mashirikisho ya michezo mbalimbali kuhakikisha mipango na mikakati wanayoweka katika kushiriki michezo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi (ya kimataifa) wanaitekeleza na waishirikishe Serikali inapobidi tuweze kufanya vizuri kwenye michuano mbalimbali.
Tunafahamu tuna vijana wamekuwa wakifanya vizuri wa Serengeti Boys, kwa hii iwe ni chachu kwao kwamba Serikali inawajali wanamichezo na tuna mambo mengi tunayafanya kwenye kutekeleza mikakati ya michezo lakini pia wafahamu pale ambapo wanatoka jasho na kufanya vizuri Serikali huwa tunawapa zawadi kuwakumbuka kama heshima kwao. Kwa hiyo kwa niaba ya Watanzania, leo tumetimiza ile ahadi, kinachobakia sasa ni kuwakabidhi hati zao kwenye shughuli ambayo tutaipanga siku chache zijazo." alihitimisha kusema Dkt Hassan Abbas.
Siku Wachezaji wa Taifa Stars walipokaribishwa Ikulu ya Dar es Salaam kupongezwa kwa ushindi wa mabao 3 - 0 dhidi ya Uganda.
Bondia Mwakinyo (mwenye suti) na baadhi ya wachezaji wa Taifa Stars wakiwa Ikulu.
Mshambuliaji wa zamani wa Taifa Stars Peter Tino akiwa na Rais Mhe. Dkt. Jonm Pombe Magufli Ikulu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.