Na. Dennis Gondwe, DODOMA
VIONGOZI wa vyama vya siasa wilayani Dodoma wametakiwa kuwahamasisha wananchi kulipa kodi na michango ili kufanikisha utekelezaji wa bajeti ya halmashauri.
Kauli hiyo ilitolewa na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Dodoma maalum kwa ajili ya kujadili rasimu ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Prof. Mwamfupe alisema kuwa vyama vya siasa vina nafasi kubwa ya kufaidi matunda ya maendeleo ya jiji. “Bila kujali chama, twende pamoja, umefika wakati wa kuwaambia wananchi wetu ukweli kwamba wanatakiwa kulipa kodi bila kujali vyama walivyopo. Nilialikwa mkutano na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wanatoa zawadi, tangu lini mtoza ushuru anatoa zawadi kwa walipa kodi? Tunataka tufike hapo na sisi tuwageukie walipa kodi wetu, tuwe tunawapa tuzo kwa kodi wanayolipa. Tuendelee kufanya hivyo, bila kujali itikadi za vyama na imani za dini tukaona kwamba tunawajibu wa kulipa kodi wananchi wetu watuelewe watakwenda mbele zaidi” alisema Prof. Mwamfupe.
Meya Prof. Mwamfupe aliwashauri wajumbe kuwa tayari kuiambia halmashauri ili iweze kutoa huduma bora kwa wananchi. “Palipo pabaya pengine tuambiwe mara mbili zaidi kuliko pazuri. Hamtatupenda kama halmashauri, kama mtatuambia mazuri tu na mabaya mkayaacha. Lakini twende na ukweli kwamba walau sasa watu wanatuelewa. Katika hoteli zetu, yamelala madawati ya wanafunzi wetu, vimelala vyumba vya wanafunzi wetu tuliona tuwekeze ili tuendelee kuvuna kwa muda mrefu” alisema Prof. Mwamfupe.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa mwaka wa fedha 2023/2024 imekadiria kukusanya na kutumia mapato yenye jumla ya shilingi 128,278,555,369 kutoka vyanzo katika vyanzo vyake vya ndani, serikali kuu, wahisani kwa ajili ya kutekeleza shughuli za maendeleo, utoaji huduma na kujiendesha.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.