VYAMA vya siasa katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma vimetakiwa kufanya kampeni za kistaarabu wiki moja kabla ya siku ya uchaguzi wa serikali za mitaa ngazi ya Mtaa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa za mwaka 2019.
Kauli hiyo ilitolewa na Msimamizi wa Uchaguzi huo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro (pichani kushoto) alipokuwa akitoa maelezo kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa ngazi ya Mitaa utakaofanyika tarehe 24 Novemba, 2019, kwa viongozi wa vyama vya siasa na Wasimamizi Wasaidizi ngazi ya Kata katika Halmashauri hiyo kwenye kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji leo.
Kimaro alisema kuwa kampeni za uchaguzi zitafanyika wiki moja kabla ya siku ya uchaguzi. “Kampeni zitafanyika kwa muda wa siku saba yaani kuanzia tarehe 17/11/2019 hadi 23/11/2019 saa 2:00 asubuhi na kumalizika saa 12:00 jioni kila siku” alisema Kimaro. Alivitaka vyama vyote kufanya kampeni za kistaarabu muda utakapofika kwa mujibu wa kanuni kwa kuzingatia maslahi mapana ya amani ya nchi.
Kuhusu uandikishaji, alisema kuwa uandikisha utafanyika kuanzia tarehe 8/10/2019 hadi 14/10/2019 kwenye vituo vya kupigia kura vilivyopo katika mitaa iliyopo kwenye orodha iliyotangazwa na serikali ya maeneo ya utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma. “Upigaji kula utafanyika kwenye vituo vya kupigia kura vilivyopo kwenye mitaa iliyoko kwenye orodha ya maeneo ya utawala ya Halmashauri ya Jiji” aliongeza Kimaro. Vituo vitafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni, aliongeza.
Msimamizi huyo wa uchaguzi alizitaja sifa za mtu anayestahili kuandikishwa kuwa awe ni raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 18 au zaidi. Sifa nyingine alizitaja kuwa ni mkazi wa eneo la mtaa husika na awe amejiandikisha kupiga kura katika Mtaa husika. Sifa nyingine mtu huyo hana ugonjwa wa akili uliothibitishwa na daktari anayetambulika na serikali au bodi ya utabibu.
Awali akimkaribisha msimamizi wa uchaguzi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Uchaguzi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Hidaya Maeda alisema kuwa kanuni za uchanguzi wa viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa ngazi ya vijiji, vitongoji na mitaa za mwaka 2019 zinaelekeza msimamizi wa uchaguzi kutoa maelezo kuhusu uchaguzi wa serikali za Mitaa utakaofanyika tarehe 24 Novemba, 2019.
Maeda alisema kuwa lengo la maelezo hayo ni kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani pasipokuwa na changamoto zozote. Akiongelea ushiriki wa maafisa watendaji wa Kata katika uchaguzi huo, aliwataja kuwa ni wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi huo ngazi ya Kata kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa za mwaka 2019.
Kikao hicho kilihudhuriwa na vyama vya siasa vya CCM, Chadema, ACT Wazalendo, UMD, Sauti ya Umma, NCCR Mageuzi, CUF na Demokrasia makini.
Sehemu ya wajumbe wa kikao cha Msimamizi wa Uchaguzi wa Jiji la Dodoma na wawakilishi wa Vyama vya siasa kutoka Jiji la Dodoma kwenye kikao kilichofanyika tarehe 23 Septemba, 2019 katika Ukumbi mkubwa wa Mikutano wa Jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.