MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Godwin Kunambi amesema Halmashauri hiyo itahakikisha watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano wanasajiliwa kwa ajili ya kupatiwa vyeti vya kuzaliwa bure kutokana na umuhimu wa nyaraka hiyo ambayo kuanzia tarehe 15 Machi, 2019 itaanza kutolewa katika Ofisi zote za Kata 41 za Jiji hilo na katika baadhi ya vituo vya kutolea huduma za Afya.
Kunambi ameyasema hayo mapema leo Machi 11, 2019, wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kuhusu usajili na utoaji wa vyeti hivyo kwa Maofisa Watendaji wa Kata, Maofisa Maendeleo ya Jamii, na Maofisa Afya watakaoshiriki katika utoaji wa vyaraka hiyo kwenye Kata husika.
Akizungumza na wataalam hao katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Umonga, Kunambi aliwataka wawajibike kikamilifu katika kufanikisha huduma hiyo kwa Wananchi ili kila mtoto mwenye haki ya kupata cheti hicho katika Jiji la Dodoma apatiwe.
“Naishukuru sana Serikali Kuu na RITA (Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini) kwa kusogeza huduma hii huku chini kwa Wananchi, sisi kama Halmashauri tutaifanya kazi hii kwa ufanisi kwani jukumu letu kubwa ni kutoa huduma kwa Wananchi” alisema Kunambi.
Kwa upande wake Mratibu wa zoezi hilo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma Aneth Mwambya alisema mafunzo hayo ni siku tatu na kuanzia Machi 11, 2019 na kwamba kuanzia Machi 15, 2019 zoezi la usajili wa watoto na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa litaanza katika ngazi ya Kata.
“Tunatoa wito kwa kila mzazi mwenye mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano wafike katika Ofisi za Kata na katika baadhi ya vituo vya kutolewa huduma za Afya zinazotoa huduma ya mama na mtoto ili wasajiliwe kwa ajili ya kupatiwa vyeti hivi vya kuzaliwa” alisema mratibu huyo.
Alisema zoezi hilo litaanza kwa kampeni ya siku 12 kuanzia Machi 15, 2019, na baada ya muda huo huduma hiyo itaendelea kutolewa kama kawaida, na kwamba kila mzazi atatakiwa kuwasilisha nyaraka za awali zikiwemo Tangazo la kuzaliwa kwa mtoto au kadi ya kliniki kabla ya mtoto husika kusajiliwa na kupatiwa cheti.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.