Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametangaza kuwa vyuo vikuu vyote nchini vitafunguliwa kuanzia Juni 1, 2020.
Wanafunzi wa kidato cha sita nchini nao ambao wanakaribia kufanya mitihani ya kumaliza elimu ya sekondari pia watarejea shuleni siku hiyo.
Rais Magufuli amesema kuwa wameamua kufanya hivyo kwa kuwa kasi ya ugonjwa wa Covid19 imepungua Tanzania.
"Hali ya ugonjwa wa Corona nchini imeshuka sana hivyo, sisi kama serikali tumeamua kufungua vyuo vyote Juni 1, 2020 kwahiyo Wizara zinazohusika zijiandae ili vyuo vitakapofunguliwa isitokee kero zingine," ameeleza Magufuli.
Magufuli hata hivyo amesema kwa wanafunzi wengine bado kunahitajika muda wa kufanya tathmini.
"Kwa shule za msingi na madarasa mengine ya sekondari tujipe muda kidogo...tutatathmini maendeleo ya wengine waliofungua kwanza. Hawa wa chuo kikuu ni watu wazima, wanajitambua," amesisitiza rais Magufuli.
Taasisi zote za elimu nchini Tanzania zilifungwa katikati ya mwezi Machi mara baada ya Tanzania kuthibitisha mgonjwa wa kwanza wa virusi vya Corona nchini.
Rais Magufuli pia ameatangaza kuwa tarehe hiyo ya Juni 1 ndiyo michezo yote ikiwemo Ligi Kuu ya Kandanda itarejea.
Michezo ni muhimu hivyo tumeamua pia kufungua michezo kuanzia Juni 1, 2020, taratibu za kuangalia na kushangilia mpira zitapangwa vizuri na Wizara ya Afya pamoja na Wizara ya Michezo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas amesema kupitia mtandao wa Twitter kuwa baada ya kauli hiyo ya rais sasa ni rasmi kwa timu zote kuanza mazoezi.
Mapema wiki hii Rais wa Shirikisho la Kandanda nchini Tanzania (TFF) Wallace Karia akiongiea na BBC alisema kuwa wanaendelea na maandalizi ya ndani wakisubiri mwongozo rasmi wa serikali.
Karia alisisitiza kuwa michezo ya ligi itakaporejea, mashabiki hawataruhusiwa uwanjani.
Aidha, Rais Magufuli pia amesema kati ya Mei 27 na 28 ndege za watalii zitaanza kuingia hapa nchini.
Hayo ameyasema asubuhi ya leo katika Ikulu ya Chamwino Dodoma kwenye hafla ya kuwaapisha viongozi kadhaa aliowateua hivi karibuni akiwemo Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel pamoja na mabalozi kadhaa.
Rais Magufuli alitangaza Jumapili iliyopita na kusisitiza hii leo kuwa kasi ya corona imepungua Tanzania.
"Kwa taarifa za leo wagonjwa wamepungua, Amana ilikuwa ina watu 198 leo wamebaki 12 tu, Mloganzila ilikuwa inalaza watu 30 leo wamebaki 6, Hospitali ya Kibaha kulikuwa na wagonjwa 50 leo wamebaki watu 22," rais Magufuli alisema siku ya Jumapili.
Mpaka sasa, watu 509 wamethibitishwa kuambukizwa virusi vya corona nchini Tanzania, huku 183 wakipona na watu 21 kufariki dunia.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.